Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa
na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye ukumbi wa Hazina jijni Dodoma, Desemba 3,
2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Wakuu wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati alipofungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa
kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Desemba 3, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Baadhi ya Makatibu Tawala wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa wakati alipofungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu
Tawala wa Mikoa kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Desemba 3, 2018. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Mfunzo
hayo yatawasaidia kusimamia utumishi na kuzingatia miiko ya uongozi
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefungua mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa
Mikoa, ambapo amesema baada ya mafunzo hayo Serikali
inatarajia watasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na wao
wenyewe watakuwa kioo katika kuzingatia miiko ya utumishi wa umma.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema viongozi hao wa mikoa watazingatia kikamilifu mipaka ya
madaraka yao na kwamba hatua watakazozichukua katika uongozi na utendaji wao
zitazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo nchini.
Waziri
Mkuu amefungua mafunzo hayo yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi leo (Jumatatu,
Desemba 3, 2018) katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo
mengine amewataka wakasimamie kikamilifu mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.
“Mkadumishe
uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa
kila mtumishi anao mchango katika kuboresha utendaji kwenye kituo chake cha
kazi. Nina matarajio makubwa kuwa mtadumisha uhusiano mzuri kikazi na viongozi
wa juu na pia uhusiano wa diplomasia ya heshima na viongozi wengine ndani ya
mihimili yetu mitatu.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wahakikishe kila mmoja wao anaandaa
mpango kazi unaoainisha shughuli zake za kila siku. “Mkuu wa Mkoa, Katibu
Tawala wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi na Wakuu wa Idara wote na
Watumishi wote wawe na mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao.”
Amesema
viongozi hao wanatakiwa wasimamie nidhamu kazini na uwajibikaji wa watumishi
kwa wananchi, ambapo pia amewasihi watende haki kwa wananchi na watumishi walio
chini yao. Pia lazima watumishi wa Serikali wawapokee na kuwahudumia wananchi
kwa staha, wawasikilize kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri
Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa waendelee kusimamia amani na utulivu
kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote
kwani amani na utulivu ndiyo itawawezesha nchi iendelee kuwavutia
wawekezaji wa ndani na nje.
“Tunakumbushwa
sisi viongozi tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya
Watanzania wote bila kubagua jinsia, kabila, dini, rangi ya ngozi, mtu atokako
ndani ya nchi ilimradi hajavunja sheria; wala ubaguzi mwingine wa aina
yoyote. Tunaaswa tuwahudumie Watanzania wote kwa usawa.”
Kuhusu
mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo, Waziri Mkuu amesema zitawawezesha
viongozi hao kupata fursa ya kutafakari na kujitathmini kuhusu hatua za
kujiimarisha zaidi kiuongozi na kiutendaji. “Hatua hizo ni lazima ziwe
pamoja na kubadilika kwa mtazamo na kujirekebisha endapo mtabaini maeneo
mliyokuwa mkikosea tangu mlipokabidhiwa ofisi hadi sasa.”
Waziri
Mkuu amesema mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinahusu majukumu na
mipaka ya kazi,ambapo watajifunza namna ya kufanya kazi bila mikwaruzano
isiyo na tija baina yao na viongozi wa mihimili mingine ya dola, viongozi wa
kisiasa na watendaji wengine Serikalini.
Amesema
mada nyingine inahusuuongozi, hisia na mahusiano mahali pa kazi, ambapo
itawawezesha kujiimarisha katika mbinu za kuwaongoza watumishi walio chini yao
kwa kujenga na kudumisha mshikamano na ushirikiano wa pamoja.
“Mada
itafafanua pia namna mnavyotegemeana na watumishi wa kada na ngazi mbalimbali
katika kutimiza majukumu yenu. Ni muhimu sana kufanya kazi kama timu moja ili
muweze kuyafikia malengo ya taasisi kwa upana wake na si malengo ya mtu au
kiongozi mmoja.”
Amesema
kwenye mada inayohusu muundo wa Serikali na namna inavyofanya kazi watauelewa
vizuri zaidi muundo wa Serikali ulivyo na jinsi unavyofanya kazi.
Pia wataielewa
vizuri zaidi itifaki na kuheshimiana kwa ngazi mbalimbali kutoka Waziri, Mkuu
wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara hadi
Wananchi.
Kwa
upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya
Uongozi, Profesa Joseph Semboja amesema mafunzo hayo ya wiki moja
yatajikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni kuimarisha uwezo wa washiriki
katika kufanya maamuzi ya kimkakati yanayozingatia mahitaji na manufaa mapana
ya sasa na ya baadae kwa jamii.
Ametaja
eneo la pili kuwa ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kuongoza rasilimali
watu na kusimamia rasilimali nyingine ili kutekeleza kikamilifu na kwa
mafanikio maamuzi ya kimkakati waliyoyafanya katika kipengele cha kwanza.
“Eneo
la tatu ni la kuimarisha uwezo wa washiriki katika kujijengea sifa binafsi za
uongozi ili awe na ushawishi kwa wananchi anaowaongoza. Hili ni jambo la
msingi, kiongozi mwenyewe awe mfano bora wa kuigwa. Awe muadilifu, mtenda haki,
mfuata sheria na taratibu pamoja na kufahamu na kuheshimu miiko ya uongozi.”
Mafunzo
hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Kapteni
Mstaafu, George Mkuchika, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt.
Binilith Mahenge na Naibu Waziri Ofisi
ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment