METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, December 25, 2018

CCM MOROGORO YAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUBORESHA HESHIMA YA TANZANIA KIUCHUMI

Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro kinatoa mkono wa kheir na baraka kwa wauminu wote wa dini ya kristo wakati huu tukisherehekea sikukuu ya Christmas aidha tunawatakia watanzania wote mapumziko ya sikukuu pamoja na kukaribisha mwaka mpya wa 2019.

Kupitia mapumziko haya Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro tumeona ni vyema kutumia siku ya leo kuzungumzia mambo kadhaa yenye muktadha na mustakabali mwema kwa Taifa letu.

Nchi yoyote duniani ili iweze kupata mafanikio yake kiuchumi, kisiasa na kijamii lazima kwanza wananchi wake wawe makini, wapende umoja, maelewano, uzalendo hatimaye wawe na sauti ya pamoja. 

Tanzania kwa miaka mingi imekuwa moja na inatakiwa kuwa moja daima, ni nchi moja kati ya nchi za Kusini mwa Afrika, ilitoa mchango mkubwa katika harakati za kupigania ukombozi kusini mwa Afrika kwa kuzisaidia nchi mbali mbali na wapigania uhuru wake hatimaye mataifa hayo sasa yako huru na kijitawala.

Chini Rais wa kwanza Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere nchi yetu ilishiriki kikamilifu harakati za kupigania uhuru wa nchi yetu hatimaye tukajitawala wenyewe mwaka 1961 kutokana na kuwa na umoja na mshikanano wa kitaifa chini ya chama cha TANU.

Mara baada ya uhuru tukafanikiwa kujenga umoja wa kitaifa, kuvunja matabaka ya ukabila, udini, kupinga siasa za ubaguzi wa rangi , ukanda, kusimamisha na kulinda misingi ya sheria na usawa iliotokana na sauti moja .

Kwa kujali kwetu na kutambua umuhimu wa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na kuthamini sauti moja , tuliziunganisha nchi zetu mbili Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 , tukaunda Taifa moja linaloitwa Tanzania ambalo halikuachwa na wakoloni .

Mwaka 1977 kwa kujali maslahi mapana zaidi ya nchi zetu , kujiongezea usalama na ulinzi wa mipaka ya Taifa letu kijamii, kisiasa na kiuchumi; wazee wetu waasisi wakapitisha maamuzi magumu ya kuvinganisha TANU na ASP na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) .

Kwa hiari yetu tuliamua kufuata Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ambapo sera zake zilianzisha Vijiji vya Ujamaa, wananchi wakapelekewa huduma muhimu za maendeleo kama za kilimo cha kisasa , ufugaji, kuwapatia elimu bure , maji, umeme na ujenzi wa nyumba na barabara, kwa nguvu ile ile ya sauti moja.

Tanzania ndiyo Taifa pekee ulimwenguni lililojitenga na ushabiki wa siasa za mkumbo wa pande mbili za Magharibi na Mashariki wakati wa iliokuwa vita baridi , ikitangaza kutofungamana na upande wowote bali itaendelea kuheshimu na kutetea misingi ya haki za binadamu, kupigania usawa na amani mahali popote duniani. 

Mwaka 1978 nchi yetu ilivamiwa na Majeshi Dikteta Idd Amini wa Uganda. Askari wake wakakalia sehemu ya Ardhi yetu na kujitangazia ni miliki yao pia wakiwaua baadhi ya wananchi wetu. Tuliitangazia dunia na kulazimika kuingia kwenye vitani hiyo huku tukiwa na mshikamano imara wenye nguvu na sauti moja.

Baada ya uvamizi huo , tukaitangazia dunia kuwa adui ametuvamia na tayari amekali eneo la nchi yetu kimabavu kinyume na haki. Mataifa kadhaa yakaamua kukaa kimya ukiwemo na uliokuwa Umoja wa Nch Huru za Afrika (OAU) kushindwa hata kumkaripia na kumuonya Dikteta Idd Amin.

Tukasema lazima tupambane na adui ili kumtoa nje ya mipaka yetu. Tukafanya hivyo na kufanikiwa kumchakaza yeye na majeshi yake , hatimaye tukamtoa kutokana na na nchi yetu na watu wake kuwa na msimamo thabiti wa sauti moja.

Nchi yetu ikabahatika kupata uongozi mwingine wa awamu ya pili , tatu na nne . Sasa tuko kwenye awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli . Bado tunatakiwa kuwa na shime ile ile ari na mshikamano ule ule huku Tanzania yetu ikitajwa ni Taifa linaloenzi Amani, Umoja , Utulivu na Maendeleo. 

Taifa letu lilifanikiwa kujenga viwanda vingi, kuanzisha mashrika ya Umma, kampuni na wakala za serikali lengo ni kujijenga kiuchumi ili nchi na watu wake wajitegemee bila kusubiri misaada, fadhila au hisani za kigeni. 

Katika juhudi hizo za serikali napenda niwe mkweli na kusema kuwa kuna mahali tulijikwaa na kujikuta tukipiga mwereka. Bila kutarajia tukarudi hatua nyingi na miaka mingi nyuma kimaendeleo na kujikuta tukiwa nchi tegemezi isozalisha wala kuuza bidhaa nje na kwenye soko la dunia.

Awamu ya tano ya utawala wa nchi yetu chini ya wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ) imechemsha bongo, imetafakari kwa kina na kupata majawabu ya kisa cha kudondoka kwetu toka mahali tulipokuwa ambako tulifikia katika kilele cha kuridhisha kimaendeleo na vipi tilirudi nyuma hadi mahali tulipo.

Serikali ya CCM chini ya uongozi mahiri na ushupavu wa Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli kwa dhati kabisa imeamua kurudisha heshima ya nchi yetu kiuchumi hatimaye tuwe Taifa linalijiendesha na kujitegemea kutokana na matumizi bora aidha ya rasilimali zake, maliasili, mito, maziwa , bahari pia ardhi huku watu wake tukitakiwa kufanya kazi kwa bidii na nidhamu .

Malengo hayo na utekelezaji wake umeanza kwa kasi. Hivi sasa tunatakiwa wananchi wote bila kujali au kutotanguliza mbele itikadi za vyama vyetu , tunao wajibu wa kumuunga mkono Rais wetu, sera za serikali kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM 2015/2020, mipango na mikakati alionayo ikiwemo dhamira njema anayoionyesha.

Ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake amefanya maajabu ambayo hayakutarajiwa. Serikali yake imeamua kulinda rasimali za Taifa na kutaka zitumike kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya watu. Amefanikiwa kusimamisha nidhamu ya kazi kwenye serikali kuu , halmshauri za wilaya , vyombo vya sheria, mamlaka, wakala za umma , taasisi , wizara na idara za serikali.

Serikali yetu imeondosha kero na tatizo sugu la kukosekana madarasa na madawati kwenye shule za msingi. Imenza kutoa elimu bure toka msingi hadi kidato cha nne. Inajenga vituo vya Afya, wodi za wagonjwa za kina mama wajawazito, uanzishaji wa mradi mkubwa wa maji toka ziwa victoria huko Mwanza hadi Mikoa ya Shinyanga , Tabora na vijiji vyake. 

Imeanzisha miradi mikubwa ya maendeleo , ujenzi wa reli ya mwendokasi inayotumia umeme , mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa maporomoko utakaotoa megawati 2100 kwenye maporomoko ya Rufiji (Steaglers Gorge) , kufufua shirika la ndege huku serikali ikinunua ndege kubwa mpya za kisasa .

Chama cha Mapinduzi Mkoa Morogoro kinatoa wito wa kuwataka wananchi wote wazalendo katika Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, tufungue masiko na macho yetu hatimaye tutazame na kuona mahali tulipotoka , tulipo sasa na kule nchi yetu inakotaka kuelekea kimaendeleo .

Huu ni wakati muafaka kwa Taifa letu na watu wake kuinga mkono serikali ya Rais Dk John Magufuli, kutokana na kuonyesha kwake nia njema ya kulileta Taifa letu mageuzi ya kiuchumi hatimaye tuweze kupata ustawi wa maendeleo.Tuanze kujiamini na kujitegemea sisi wenyewe huku tukisiburi misaada kidogo toka kwa washirika wetu wa maendelo na jumuiya ya kimataifa.

Kimsingi tunahitahi kuendeleza na kudumisha mshikamano wetu, umoja wa kitaifa na utulivu ili kupata sauti moja yenye nguvu bila kughilibiwa na mataifa ya nje au na baadhi ya wanasiasa wa ndani wanaoshiriki siasa za ushabiki ambazo zimeweza kuleta madhara, maafa na majanga maaneno kadhaa Barani Afrika.

Siasa mapepe na ushabiki njaa, uchochezi, ukuwadi wa kisiasa na umangimeza hautatunufaisha na kutufikisha popote kimaendelo. Kuendelea kushabikia siasa za uchochezi au ugombanishi , tuelewe huko ni kupalilia mgawanyiko kwenye nchi yetu .

Tutakapokubali kuingia kwenye ngoma hiyo, tusishangae siku moja tutajikuta tuko kwenye dimbwi la majuto kama yanayowakuta wenzetu huko Libya, DRC , somali na ilivyowahi kutokea huko Burundi na Rwanda. 

Tuna haki na wajibu wa kuwa wazalendo wa kweli, tusiwe tayari kuyumbishwa na wanasiasa maslahi ambao wana matarajio ya kufikia ndoto za kushika madaraka ya utawala huku wakiwa hajali kutokea kwa madhara au hasara zinazoweza kuwakumba wananchi wanyonge, masikini na wasio ma hatia. 

Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro tunawahimiza wananchi wote kuwa wazalendo, wapenda amani , umoja na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.Tumuombe afya na maisha yenye uzima Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli ili aweze kutuongoza kwa haki na usawa hatimaye mungu mtukufu amsaidie ili aendelee kutukunjulia busati la maendeleo ya kiuchumi. 

Tuendelee kumuunga mkono na kumtia nguvu Mhe Rais wetu huku tukithamini kazi kubwa anayoifanya ndani ya Taifa letu ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Wito wetu kwa watanzania popote pale walipo kuzidisha bidii ya kazi na uzalishaji tunapokuwa aidha maofisini, viwandani au mashambani sambamba na kuwataka wananchi, viongozi , wanaharakati na wanasiasa, tusiwe wepesi wa kurubuniwa , kununuliwa utu wetu na kushiriki usaliti, lazima tujue hakuna mtu mwingine atakayetuonyesha hatma ya nchi yetu ikiwa tutakubali kulibomoa Taifa letu kwa mikono yetu.

Ahsanteni

Kidumu Chama Cha Mapinduzi 

Innocent Kalogelensi(MNEC)
Mwenyekiti wa CCM 
Mkoa wa Morogoro

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com