METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 25, 2018

SERIKALI IMEANDAA MPANGO WA KUPUNGUZA UKATILI –MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Kampeni ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili  wa Kijinsia kwenye  Uwanja  wa Jamhuri jijini Dodoma, Novemba  25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wapili kulia), Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto)  na   Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la  Wanawake Katika Sheria  na Maendeleo Barani Afrika ( WILDAF), Anna Kulaya  wakati alipowasili kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuzindua Kampeni ya Siku  16 ya Kupinga Ukatili  wa Kijinsia, Novemba 25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri mkuu)
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozindua kampeni ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Novemba 25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Ni dhiri ya wanawake na watoto katika jamii kwa silimia 50 ifikapo 2022

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022. 

Amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998).

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Novemba 25, 2018) wakati akizindua Kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia katika Uwanja vya Jamhuri jijini Dodoma. Amesema katika kukabialia na ukatili wa kijinsia Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imekuwa ikichukua hatua mbalimbaliza kuzuia na kutokomeza ukatili.

Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mpango huo utachangia katika utekelezaji wa mipango na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki na ustawi wa mtoto.

Kadhalika Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza Wakuu wa Mikoa wote wahakikishe wanasimamia uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto za ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto. 

“Vilevile, nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuanzisha Programu za Kijamii za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika Halmashauri husika zitakazozingatia hali halisi na kuzitengea bajeti programu hizo kama inavyoelekezwa kwenye Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto. “

Pia Waziri Mkuu amesema watu wenye ulemavu wana mahitaji maalumu na ni wahanga wa ukatili wa kijinsia ameelekeza Jeshi la Polisi kuboresha Dawati lake la jinsia ili liweze kushughulikia kikamilifu masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watu wenye ulemavu. “Hivyo, kuanzia sasa Dawati hilo liitwe Dawati la Polisi la Jinsia, Watoto na Watu wenye Ulemavu.” 

Akizungumzia kuhusu maana ya ukatili wa kijinsia amesema ni hali ya kutenda vitendo viovu, vinavyodhalilisha, vinavyotesa, vinavyonyanyasa, vinavyokandamiza, visivyojali haki za kuishi kwa binadamu anaweza kuwa wa kiume au kike.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema ukatili wa kijinsia huja katika taswira nyingi. “Aidha, kwa uchache tunapozungumzia ukatili wa kijinsia tunamaanisha vitendo kama vile, vipigo, ubakaji, ukeketaji, ulawiti, matusi, lugha na vitendo vya udhalilishaji pamoja na kunyimwa fursa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi.”

“Hivyo, ukatili wa kijinsia ni unyanyasaji wowote unaofanywa na mtu dhidi ya mtu mwingine bila kujali umri, maumbile, kabila, rangi, dini au mtazamo wa kisiasa. Unyanyasaji huu unahusisha mambo mengi kama kumpiga mwanamke au mwanamme, kumnyima mtoto elimu, kumlawiti mtoto wa kike au kiume, kumbagua mtu katika mahitaji ya msingi au kuwanyima urithi warithi wanaohusika.”

Aidha, taarifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) za mwaka 2017 zinaonesha kuwa wanawake na wasichana wapatao milioni 750 Duniani waliolewa wakiwa chini ya miaka 18. Halikadhalika, taarifa hiyo inakadiria kuwa wasichana milioni 120 (yaani mmoja kati ya wasichana 10) Duniani wamekumbana na vitendo vya kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao. 

Waziri Mkuu amesema kama zilivyo nchi nyingine Duniani, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo la ukatili wa kijinsia na kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2015/2016 kupitia inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 - 49 wamefanyiwa ukatili wa kupigwa au kingono katika kipindi cha maisha yao. 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com