Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akiwa katika kiwanda kinachozalisha nyaya za umeme cha Everwell cable kilichopo Mkuranga mkoani Pwani. Wengine katika picha ni viongozi wa kiwanda hicho pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati, TANESCO na REA.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tano kushoto) akizungumza na watendaji wa TANESCO mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Dege wilayani Kigamboni.
Baadhi ya mitambo ya umeme katika Kituo cha kupoza umeme cha Kurasini ambacho Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameagiza kuwa kianze kufanya kazi ndani ya miezi miwili.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na
uzalishaji wa nyaya za umeme unaofanyika katika kiwanda cha Everwell Cable
& Engineering kilichopo mkoani Pwani ambacho kina uwezo wa kuzalisha nyaya
za urefu wa kilometa 24,000 kwa mwaka.
Alieleza hayo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani na Dar es Salaam
ambapo alikagua uzalishaji wa nyaya katika kiwanda hicho pamoja ujenzi wa vituo
vya kupoza umeme vya Dege na Kurasini.
“ Kwa sasa kuna viwanda vitano vinavyozalisha nyaya za kutosha na za
ukubwa mbalimbali hivyo bado nasisitiza agizo la Serikali la kutonunua nje ya
nchi vifaa vya umeme vinavyopatikana hapa nchini,” alisema Dkt Kalemani.
Aidha, Dkt Kalemani alisema kuwa, Serikali haitawavumilia wakandarasi au
wataalam wanaochelewesha utekelezaji wa miradi ya umeme kwa kisingizio cha
kutokuwa na vifaa wakati vinapatikana kwa wingi na gharama nafuu ukilinganisha
na vifaa kutoka nje ya nchi.
Akiwa katika kituo cha kupoza umeme cha Dege wilayani Kigamboni,
alieleza kuridhishwa na hatua za ujenzi zilizofikiwa hadi sasa lakini alitoa
agizo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa
ujenzi wa kituo hicho unakamilika ifikapo Februari mwaka 2019 badala ya Oktoba,
mwakani.
Alisema kuwa kituo hicho kitafungwa mashine zenye uwezo wa megawati 200
lakini itaanza kufungwa mashine moja yenye uwezo wa megawati 50 itakayohudumia
eneo la Kigamboni ambalo mahitaji yake ya umeme ni chini ya megawati 25.
Vilevile, Dkt Kalemani alikagua ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha
Kurasini na kupongeza TANESCO kwa kukamilisha ujenzi wa Kituo hicho ambacho
kimefungwa mashine yenye uwezo wa megawati 40 itakayoimarisha upatikanaji wa
umeme katika maeneo ya Kurasini na Kigamboni.
Dkt. Kalemani alisema kuwa, mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2009,
ulikuwa ukisuasua kutokana na wakandarasi kutotekeleza majukumu yao kwa ufanisi
na kwa sasa kuna mwananchi mmoja amekataa kupisha moja ya eneo inakopita
miundombinu ya umeme kwa kukataa fidia ya milioni 800.
Kuhusu suala hilo la fidia, Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa TANESCO
kufanya mazungumzo na mwananchi huyo kwani atalipwa fedha hizo kwa mujibu wa
viwango vya Serikali na ndani ya miezi miwili kituo hicho kianze
kufanya kazi.
0 comments:
Post a Comment