METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 20, 2018

WAZIRI MKUU ATOA SIKU 25 KWA WATUMISHI CHAMWINO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa barabara za mitaa katika mji wa Chamwino zinazojengwa kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 3.5, Oktoba 20, 2018. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa na watatu kushoto ni Mbunge wa Chilonwa, Joel Mwaka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mashine za kusukuma  maji ya umwagiliaji wakati alipotembelea shamba la zabibu katika kijiji cha  Chinangali wilayani Chamwino, Oktoba 20, 2018. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shamba la zabibu katika kijiji cha Chinangali wilayani Chamwino, Oktoba 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia ngoma ya asili ya kabila la Wagogo wakati alipowasili katika kijiji cha Mpwayungu wilayani Chamwino kuakagua ujenzi wa Kituo cha Afya na kuhutubia mkutano wa hadhara, Oktoba 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Ni wale washio nje ya kituo, wawe wamehamia ifikapo Desemba 15  

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaametoa siku 25 kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Chamwino wanaoishi nje ya kituo chao cha kazi wawe wamehamia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza pia kuwa amemkabidhi Mkuu wa wilaya hiyo Bibi Vumilia Nyamoga orodha ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Chamwino ambao wanaishi nje ya kituo cha kazi kwa hatua zaidi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba 20, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Chamwino.

“Ifikapo Desemba 15 mwaka huu watumishi wote wawe wamehamia katika kituo chao cha kazi. Sheria ya utumishi inamtaka mtumishi aishi katika maeneo ya kituo cha kazi.”

Waziri Mkuu amesema lazima watumishi wote wa umma wafuate sheria, kanuni na taratibu za utumishi na atakayeshindwa kuhamia atakuwa amejiondoa kwenye utumishi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wakuu wa idara na madiwani watambue vyanzo vyote vya mapato.

Amesema baada ya kuvitambua wasimamie utaratibu wa ukusanyaji kwa njia ya kielekroniki ili kuiwezesha halmashauri kupanga miradi na kuitekeleza kupitia fedha za ndani.

Pia Waziri Mkuu amekagua barabara za mitaa katika mji wa Chamwino zenye urefu wa kilomita 3.5 zinazojengwa kwa kiwango cha lami na kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo.

Baada ya kukagua barabara hizo, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa miundombinu ya majengo ya kituo cha Chamwino na kisha kuzungumza na wananchi waliofika  kituoni hapo. 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com