Na Munir Shemweta,
WANMM Kilimanjaro
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesuluhisha mgogoro uliodumu zaidi ya miaka
thelathini ambao ulileta uhasama na chuki baina ya Shirika la
Watawa wa Kikatoliki na wananchi wa kijiji cha Mlongoni katika
Wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro kuhusiana na shamba la Kirari.
Katika shamba hilo wananchi wa
kijiji cha Mlongoni wanaishi katika eneo lenye ukubwa wa ekari 347 na Watawa
kubakia na ekari 1063 ambapo kwa mara ya kwanza Hati ya shamba hilo ilitolewa
tarehe 26 Oktoba, 1950 kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo.
Lukuvi alifikia suluhu na pande
hizo mbili baada ya kukutana na Watawa wa Katoliki na baadaye viongozi wa
kijiji cha Mlongoni kwa lengo la kutafuta suluhu baada ya Mahakama ya Rufaa
Tanzania kuwapatia ushindi Watawa na hivyo kulazimu wananchi wa kijiji hicho
wanaofikia 3,700 kutakiwa kuondoka katika shamba la Kirari.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi aliamua kuenda eneo hilo la kijiji cha Mlongoni jana wakati
akiwa katika ziara yake ya kutembelea wilaya za Hai, Moshi na Same mkoa wa
Kilimanjaro kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya hizo.
Katika kikao chake na Watawa wa
Katoliki, Lukuvi aliwaeleza kuwa Shirika lao ni wamiliki halali wa shamba hilo
kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa na Serikali haiwezi kupingana na
maamuzi ya Mahakama na kusisitiza anachotaka yeye ni kuangalia namna bora ya
kutekeleza hukumu ya Mahakama.
Aliwaeleza Watawa kuwa, pamoja
na wao kupatiwa ushindi katika kesi hiyo kuna haja ya wao kuangalia
namna bora ya utekelezaji wa hukumu hiyo bila kuathiri wananchi wanaoishi eneo
hilo ambao wengi wameishi kwa muda mrefu wengine wakiwa wameuziwa maeneo bila
ya kufahamu.
“Ninyi ni wamiliki halali wa
eneo hilo kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa lakini ili kuweza kufanya
kazi kwa amani kwenyea eneo hilo ni lazima kutafuta namna bora ya kutekeleza
uamuzi wa mahakama, ni lazima kuwe na win win situation” alisema Lukuvi
Haikuwa kazi rahisi kuweza
kuwashawishi Watawa kukubaliana na ombi la Lukuvi lakini baada ya kutumia takriban
saa mbili kuwaelewesha namna alivyoweza kushughulika na migogoro ya aina hiyo
zaidi ya 120 katika maeneo tofauti ya nchi, Watawa walikubali kumuachia
kushughulikia utekelezaji bora wa hukumu ya mahakama .
Uamuzi huo wa Watawa ulimfanya
Lukuvi kuenda eneo la tukio wilayani Siha na kukutana na uongozi wa kijiji cha
Mlongoni na baadaye wananchi wote wa kijiji hicho.
Katika mazungumzo yake na
wananchi wa kijiji hicho, Lukuvi aliwaeleza kuwa kufuatia hukumu ya Mahakama ya
Rufaa, wananchi hao hawana haki ya kuwepo eneo hilo na Serikali haiwezi
kuingilia uamuzi huo na katika kutekeleza maamuzi ya Mahakama wananchi
wanatakiwa kuondoka kwenye shamba hilo ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao.
Hata hivyo, Lukuvi aliwaeleza
wananchi hao kuwa, Serikali ya awamu ya tano ni Serikali inayowajali wanyonge
hivyo haitakuwa busara kuwaondoa wananchi wanaokadiriwa kufikia 3,700 hasa
ikizingatiwa baadhi yao walijenga nyumba kwa kuweka fedha kidogo kidogo.
Katika kutekeleza namna bora ya
hukumu ya Mahakama, Lukuvi aliwaeleza wana kijiji kuwa ili suala hilo liishe
kwa usalama na amani ni vyema wakakubaliana na utaratibu utakaopangwa na
Serikali na hatua ya kwanza ni kufanya tathmini katika eneo hilo kwa lengo la
kujua idadi halisi ya wakazi pamoja na mali zao ili kuepuka wajanja wachache
wanaoweza kujipenyeza kwa nia ya kujinufaisha na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya
Siha na timu yake kuanza kazi hiyo mara moja.
Aidha, katika kushughulikia
suala hilo Lukuvi alisitisha uendelezaji wowote katika eneo hilo hadi hapo
utaratibu mzuri utakapofanywa na kufafanua kuwa uendelezaji wowote
utakaofanyika unaweza kuleta athari kwa wana kijiji ambao kwa sasa hawana haki
na eneo hilo.
Mwenyekiti wa kijiji cha
Mlongoni Manase Herman alimshukuru Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kwa jitihada zake za kutafuta suluhu katika mgogoro huo uliodumu kwa
zaidi ya miaka thelathini na kubainisha kuwa wao kama viongozi wa kijiji cha
Mlangoni wanakubaliana na utaratibu utakaotumiwa na Lukuvi katika kutafuta
suluhu ya jambo hilo huku mwananchi mwingine John Ngwandi akitaka serikali
kuangalia namna ya kuwasaidia hasa ikizingatiwa kizazi cha awali kilishatoweka
na wengi waliobaki ni wa kuanzia miaka ya sitini.
0 comments:
Post a Comment