Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia) na Mbunge wa Mkinga, Dunstan Kitandula wakipongezana mara baada ya Mbunge huyo kukabidhiwa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) vitakavyotumika kuunganishia umeme wananchi wa Kijiji cha Magaoni wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (mwenye kipaza sauti) akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kibiboni wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga ambapo pia alizindua huduma ya umeme katika Kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuanza kupatikana kwa umeme katika Kijiji cha Magaoni wilayani Mkinga mkoani Tanga, kushoto kwake ni Mbunge wa Mkinga, Dunstan Kitandula.
Baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Magaoni mkoani Tanga.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewataka wakandarasi
wanaosambaza umeme vijijini kutoficha vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) wakati wa
usajili wa wananchi wanaohitaji kuunganishwa na huduma hiyo.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani, aliyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi
mkoani Tanga ambapo alizindua huduma ya umeme katika kijiji cha
Magaoni na Kibiboni vilivyopo wilayani Mkinga na Kijiji
cha Tingeni na Kwabota vilivyoko wilayani Muheza.
“ Ni marufuku kwa mkandarasi kuficha vifaa vya Umeta wakati wa
usajili wa wananchi, hakikisheni vifaa hivi vinakuwepo na mwananchi awe
huru kuchagua kama anahitaji kuunganishiwa umeme kwa kutumia UMETA au kuingia
gharama ya kutandaza nyaya ndani ya nyumba yake,”alisema Dkt Kalemani.
Alisema kuwa, kila mkandarasi amepewa vifaa vya Umeta
250 kwa kila eneo lake la mradi hivyo wana wajibu wa kuhakikisha kuwa, wananchi
wanafahamu uwepo wa vifaa hivyo ili kuwapunguzia gharama za kutandaza nyaya
ndani ya nyumba.
Katika mikutano yake na wananchi, Dkt Kalemani aliwahamasisha
kutumia vifaa hivyo kwani Mkandarasi anapomaliza idadi ya Umeta aliyokabidhiwa
na Serikali, vifaa hivyo huuzwa kwa bei ya shilingi 36,000 .
Dkt Kalemani pia aliwaagiza wakandarasi wa
umeme vijijini, kuhakikisha kuwa wanakuwa na wafanyakazi wa kutosha
katika maeneo yao ya mradi ili kutochelewesha kazi ya usambazaji umeme.
Vilevile alitoa wito kwa Wenyeviti wa Halmashauri na
Vijiji kuhakikisha kuwa wanatenga fedha kiasi cha shilingi 27,000
kwa ajili ya kulipia huduma ya kuunganisha umeme katika Taasisi za umma kama
shule na vituo vya afya.
Aliongeza kuwa, Taasisi za Umma zenye vyumba
vichache zinaweza kuunganishwa na huduma ya umeme kwa kutumia kifaa
cha Umeta ikiwemo Ofisi za Vijiji na Vituo vya Polisi.
Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka wakandarasi wanaosambaza
umeme vijijini kuhakikisha kuwa wanaajiri vijana katika maeneo
wanayofanyia kazi ili kutengeneza ajira katika maeneo hayo .
Katika ziara hiyo, Dkt Kalemani aliambatana na Mbunge wa
Mkinga, Dunstan Kitandula na Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu
ambao pamoja na kueleza changamoto za usambazaji umeme katika maeneo yao,
walipongeza jitihada zinazoendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka
2021 wananchi wote wanapata huduma ya umeme.
0 comments:
Post a Comment