Friday, October 5, 2018

Wakandarasi wa Umeme Vijijini watakiwa kutoficha vifaa vya Umeta


Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia) na Mbunge wa Mkinga, Dunstan Kitandula wakipongezana mara baada ya Mbunge huyo kukabidhiwa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) vitakavyotumika kuunganishia umeme wananchi wa Kijiji cha Magaoni wilayani Mkinga mkoani Tanga.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (mwenye kipaza sauti) akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kibiboni wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga ambapo pia alizindua huduma ya umeme katika Kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuanza kupatikana kwa umeme katika Kijiji cha Magaoni wilayani Mkinga mkoani Tanga, kushoto kwake ni Mbunge wa Mkinga, Dunstan Kitandula.
Baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Magaoni mkoani Tanga.


Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewataka wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini kutoficha vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) wakati wa usajili wa wananchi wanaohitaji kuunganishwa na huduma hiyo.

Waziri wa Nishati,  Dkt Medard Kalemani,  aliyasema hayo akiwa katika  ziara ya kikazi mkoani Tanga ambapo alizindua  huduma ya umeme katika kijiji cha Magaoni na Kibiboni vilivyopo wilayani  Mkinga na  Kijiji cha Tingeni  na Kwabota vilivyoko wilayani Muheza.

“ Ni marufuku kwa mkandarasi kuficha vifaa vya Umeta wakati wa usajili wa wananchi, hakikisheni vifaa hivi vinakuwepo na mwananchi awe huru kuchagua kama anahitaji kuunganishiwa umeme kwa kutumia UMETA au kuingia gharama ya kutandaza nyaya ndani ya nyumba yake,”alisema Dkt Kalemani.

Alisema kuwa,  kila mkandarasi amepewa vifaa vya Umeta 250 kwa kila eneo lake la mradi hivyo wana wajibu wa kuhakikisha kuwa, wananchi wanafahamu uwepo wa vifaa hivyo ili kuwapunguzia gharama za kutandaza nyaya ndani ya nyumba.

Katika mikutano yake na wananchi, Dkt Kalemani aliwahamasisha kutumia vifaa hivyo kwani Mkandarasi anapomaliza idadi ya Umeta aliyokabidhiwa na Serikali, vifaa hivyo huuzwa kwa bei ya shilingi 36,000 .

Dkt Kalemani pia aliwaagiza  wakandarasi  wa umeme vijijini, kuhakikisha  kuwa wanakuwa na wafanyakazi wa kutosha katika maeneo yao ya mradi ili kutochelewesha kazi ya usambazaji umeme.

Vilevile  alitoa wito kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Vijiji  kuhakikisha kuwa wanatenga fedha kiasi cha shilingi 27,000 kwa ajili ya kulipia huduma ya kuunganisha umeme katika Taasisi za umma kama shule na vituo vya afya.

Aliongeza kuwa, Taasisi za Umma  zenye vyumba vichache  zinaweza kuunganishwa na huduma ya umeme kwa kutumia kifaa cha Umeta ikiwemo Ofisi za Vijiji na Vituo vya Polisi.

Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka wakandarasi  wanaosambaza umeme vijijini kuhakikisha kuwa  wanaajiri vijana katika maeneo wanayofanyia kazi  ili kutengeneza ajira katika maeneo hayo .

Katika ziara hiyo, Dkt Kalemani aliambatana na Mbunge wa Mkinga,  Dunstan Kitandula na Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu ambao pamoja na kueleza changamoto za usambazaji umeme katika maeneo yao, walipongeza jitihada zinazoendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2021 wananchi wote wanapata huduma ya umeme.

No comments:

Post a Comment