Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akimkabidhi nakala ya
Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa huo Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati wa Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo
(SIDO) yaliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani
humo,kuanzia Oktoba 23 na kuhitimishwa Oktoba 28, 2018(kulia) Balozi wa
Nigeria nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Shahabi Issa Gada.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage
akizungumza na wajasiriamali mara baada ya kutembelea mabanda yao katika Kilele
cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu
katika Viwanja vya Nyakabindi,kuanzia Oktoba 23 na kuhitimishwa Oktoba
28, 2018.
Waziri wa Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akizungumza na baadhi ya viongozi wa World
Vision na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima alipotembelea banda lenye bidhaa za
sabuni zinazozalishwa kupitiakiwanda kidogo kilichopo wilayani Itilima, katika
Kilele cha Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani
Simiyu katika Viwanja vya Nyakabindi, kuanzia Oktoba 23 na kuhitimishwa
Oktoba 28, 2018.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.
Charles Mwijage amesema viwanda vidogo na vya kati vina mchango mkubwa katika
uchumi, maendeleo na ustawi wa nchi yoyote, kwa kuwa vinatoa ajira kwa
watu wengi ikilinganishwa na viwanda vikubwa hivyo havipashwi kubezwa kwa namna
yoyote.
Mhe. Mwijage ameyasema hayo Oktoba 28, 2018 wakati
akihitimisha Maonesho ya Viwanda Vidogo Kitaifa yaliyofanyika Kitaifa kwa mara
ya kwanza katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu kuanzia Oktoba 23.
“ Najua kuna watu wanapenda kubeza lakini napenda
niwaeleze nafasi ya viwanda na biashara ndogo katika uchumi, maendeleo na ustawi
ya nchi yoyote, Sisi Tanzania tangu uhuru mpaka leo tuna viwanda 54,000, lakini
asilimia 99 ni viwanda vidogo, vidogo sana na vya kati; sisi siyo kilema kwenye
viwanda nchi zote zipo hivyo, viwanda vyenye tija na vinavyoajiri watu
wengi ni viwanda vidogo, vidogo sana na vya kati” alisema Mwijage.
Amesema pamoja na viwanda
vidogo na vidogo sana kuwa na tija katika uchumi wa nchi viwanda hivyo pia ni
shule na vinaweza kumilikiwa kirahisi huku akisisitiza kuwa lengo la Serikali
ni kujenga uchumi jumuishi ambao nji rahisi ya kuufikia ni kupitia uchumi wa
viwanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO), Prof.Sylvester Mpanduji
ametoa wito kwa Watanzania kuwa, ili waweze kushiriki katika Ujenzi wa Uchumi
waViwanda hawana budi kuanza na viwanda vidogo ambavyo SIDO itakahakikisha
vinakuwa endelevu.
Akizungumzia Maonesho ya
Viwanda Vidogo Prof. Mpanduji amesema yamesaidia kuwaleta wajasiriamali pamoja
kuonesha bidhaa zao na kubadilisha uzoefu katika teknolojia, usindikaji na
masuala mengine yanayohusu bidhaa wanazozalisha kupitia viwanda vidogo na vya
kati.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.
Anthony Mtaka amesema mkoa huo umebeba ajenda ya Tanzania ya viwanda huku
akibainisha kuwa mwaka 2019 Simiyu imedhamiria Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli atakapotembelea mkoa huo afanye
uzinduzi wa Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa Moja kwa kufungua kiwanda
katika kila wilaya.
Aidha, Mtaka amemhakikishia
Waziri Mwijage kuwa Simiyu itaongeza uzalishaji wa malighafi ya viwanda hapa
nchini mara mbili na kuomba wizara ya viwanda isaidie upatikanaji wa teknolojia
za viwanda kuja nchini.
Akizungumzia dhamira ya
kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika Ujenzi wa Uchumi wa viwanda
Mkurugenzi Msaidizi wa UNDP anayeshughulikia miradi Amoni Manyama, amesema
Shirika hilo liko tayari kushirikiana na Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine
nchini, katika nyanja ya kifedha na kitaalam kwa kufanya uchambuzi wa viwanda
vinavyowezekana katika mikoa mbalimbali.
Maonesho ya Viwanda Vidogo
ambayo yamefanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza, chini ya kauli mbiu “PAMOJA
TUJENGE VIWANDA KUFIKIA UCHUMI WA KATI” yameshirikisha
wajasiriamali 515 kutoka mikoa 23 hapa nchini na nchi jirani za Burundi na
Uganda, ambapo pia Mabalozi kutoka nchi za Nigeria na Angola walishiriki.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment