Na Teresia Mhagama, Kilombero
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ameagiza kuwa gharama ya kuunganishia umeme wananchi kwa miradi ya umeme vijijini, iwe binafsi au ya Serikali ni shilingi 27,000 tu kama ilivyo kwa miradi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Ofisi ya Morogoro, kabla ya kufanya ziara ya kukagua mitambo ya kuzalisha umeme ya Kidatu, kufungua Ofisi mpya ya TANESCO na kuzindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Katurukila wilayani Kilombero.
“Kwa mfano kuna kampuni moja binafsi inatoza gharama ya umeme kwa kuangalia idadi ya balbu zilizopo kwenye nyumba, hili halikubaliki na ninatoa agizo kuwa, wananchi wa vijijini wanapaswa kulipia shilingi 27,000 tu, anayekubaliana na agizo hili apewe mradi na asiyekubali asiepewe kazi ya kusambazia umeme wananchi,” alisema Dkt kalemani.
Alieleza kuwa, ili suala hilo litekelezwe kwa ufanisi, atafanya kikao na waendelezaji wa miradi ya umeme vijijini ili kuwaeleza msimamo wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani amewataka wadaiwa sugu wa bili za umeme wahakikishe kuwa madeni yao yanalipwa ndani ya mwezi Novemba mwaka huu, la sivyo, TANESCO itaendelea kukata umeme kwa watu binafsi au Taasisi za Serikali zinazodaiwa madeni hayo.
“ TANESCO pia mnapaswa kufuatilia wadaiwa wenu ili kuhakikisha kuwa wanawalipa kwa wakati, hakikisheni kuwa mnakuwa na Afisa maalum wa kufuatilia madeni na mtu asipolipa akatiwe umeme,” alisema Dkt Kalemani.
Aidha, aliagiza kuwa, Ofisi zote za TANESCO nchini ziwe na stoo kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya umeme kama mita, vikombe, nguzo, na nyaya ili endapo kunatokea tatizo katika mitambo ya uzalishaji umeme au miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme, kunakuwa na utatuzi wa haraka.
“ Lazima kuwe na stoo ya vifaa mbalimbali vya umeme na kuanzia mwezi Januari, mwakani nitakagua ofisi zote za TANESCO ili kujihakikishia kama mnatekeleza agizo hili ambalo litatatua changamoto ya wananchi kukosa umeme kwa muda mrefu mara inapotokea hitilafu kwa sababu tu ya kukosa kifaa,” alisema Dkt Kalemani.
Akiwa wilayani Kilombero, Dkt Kalemani alizindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Katurukila ambacho kimeunganishwa na huduma hiyo kupitia mradi wa ubunifu wa miundombinu ya umeme ya gharama nafuu (LCD) ambao ni mradi wa majaribio uliogharamiwa na Serikali kupitia REA.
Dhana ya mradi huo wa bei nafuu ni kupunguza gharama za ujenzi kwa kufanya ubunifu unaotofautisha mradi huo na miradi mingine ya kawaida ya usambazaji umeme mfano kutumia njia mbili za umeme wa msongo wa kV 33 badala ya tatu, kutumia mbao badala ya vyuma vya kushikia vikombe na nyaya pamoja na transfoma kufungwa katika nguzo za kawaida za kupitishia umeme badala ya nguzo maalum.
Vilevile, Dkt Kalemani alifungua ofisi mpya ya TANESCO wilayani Kilombero ambayo itawawezesha wataalam wa Shirika hilo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwemo uhudumiaji wa wateja.
Ofisi hiyo imejengwa na wataalam wa TANESCO kupitia kitengo cha ujenzi ambapo wataalam hao wamejenga jengo hilo kwa gharama ya shilingi milioni 270.2 badala ya milioni 500 ambazo mkandarasi binafsi alizihitaji ili kujenga jengo husika.
0 comments:
Post a Comment