Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Bernard
makali (Kulia) akimkabidhi mkataba wa kusambaza dawa na vifaa tiba kwa mkoa wa
Rukwa kwa Mkurugenzi wa Maranatha Pharmacy Ltd. Bw. Stephen Lengeni (kushoto)
Serikali kupitia ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa imeanzisha mfumo wa Jazia Prime vendor kwaajili ya kupata
dawa na vifaa tiba pale vinapokosekana katika Bohari ya Dawa (MSD), mfumo ambao
unakuwa na mzabuni mmoja atakayesambaza dawa na vifaa tiba ndani ya mkoa mzima.
Kupitia utaratibu huo Ofisi ya mkuu wa mkoa wa
Rukwa kupitia katibu tawala wa mkoa Bernard Makali wamewekeana saini na mzabuni
ambaye ni kampuni ya Maranatha Pharmacy Ltd, atakayesambaza dawa na vifaa
tiba hivyo kuanzia katika ngazi ya zahanati katika halmashauri nne za mkoa, ili
kuongeza upatikanaji wake.
Akifungua hafla hiyo fupi ya kuwekeana saini mkuu
wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa mfumo huo utawezesha na
kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu pale ambapo vitakuwa
havipatikani MSD
“Mfumo huu unaendeshwa kwa kumlipa mzabuni fedha
mara tu baada ya vituo husika kuchukua dawa na vifaa tiba na si kwa mkopo.
Maana yake vituo vya kutolea huduma za afya vinatakiwa kuhakikisha vina fedha
kabla ya kupeleka mahitaji yao kwa mzabuni,” Alisema.
Aidha alitoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri
kuhakikisha wanasimamia vyema mapato na matumizi ya fedha kutoka katika vyanzo
mbalimbali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha fedha
zilizotengwa kwaajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba zinatumika kwa mujibu wa
miongozo iliyopo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Maranatha Pharmacy
Ltd alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuiamini kampuni yake ambayo hadi
sasa imeingia mikataba na mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya pamoja na Rukwa ambapo
mara ya mwisho kufanya kazi na serikali ilikuwa mwaka 2006 wakati ambao mifumo
ilikuwa haiku sawa.
Mbali na kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa mfumo
huu unatarajiwa kuboresha huduma kwa wazee, ambapo mkoa una jumla ya wazee 14,832
waliopatiwa vitambulisho vya kupatiwa matibabu bure.
0 comments:
Post a Comment