METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, September 7, 2018

UPOTEVU WA CHAKULA BAADA YA KUVUNA BADO TATIZO KUBWA BARANI AFRIKA-DKT TIZEBA

Waziri wa kilimo-Tanzania Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akizungumza juu ya upunguzaji wa upotevu wa chakula wakati wa hotuba yake kwenye mkutano wa Mapinduzi ya kijani Barani Afrika (African Green Revolution Forum-AGRF) unaofanyika kwa siku nne unaofanyika Mjini Kigali nchini Rwanda kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2018 mjini Kigali nchini Rwanda. (Picha Na Mathias Canal,WK)

Na Mathias Canal, Kigali-Rwanda

Imebainika kuwa Barani Afrika, upotevu wa chakula bado ni changamoto kubwa inayohitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwani zaidi ya asilimia 30% ya chakula hupotea huku kwa uoande wa mbogamboga na matunda, upotevu ni wa juu zaidi kwani inakadiriwa kufikia asilimia 50% au zaidi.

Upotevu wa chakula una matokeo hasi katika uhifadhi wa chakula ambapo ni tatizo la dunia nzima linaloathiri jamii kwa mtu mmoja mmoja na bara la Afrika kwa ujumla wake. Kutokana na takwimu za Shirika la chakula duniani, asilimia 30% ya chakula kinachozalishwa kwa matumizi ya binadamu hupotea katika mchakato wa usambazaji kila mwaka. 

Hayo yamebainishwa Jana tarehe 6 Septemba 2018 na Waziri wa kilimo-Tanzania Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba wakati wa hotuba yake kuhusu mada juu ya upunguzaji wa upotevu wa chakula kwenye mkutano wa Mapinduzi ya kijani Afrika (African Green Revolution Forum-AGRF) unaofanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2018 mjini Kigali nchini Rwanda.

Alisema kuwa hali hiyo inamaanisha makadirio ya Tani bilioni 1.3 ya chakula hayamfikii mlaji wa mwisho. Upotevu huu wa mazao hujumuisha upotevu wa rasilimali za uzalishaji, kama vile ardhi, maji, nishati na hatimae upotevu wa kipato kwa watu wote katika mnyororo wa uzalishaji na usambazaji.

Dkt Tizeba alisema kuwa nchini Tanzania, pamoja na kuwa kumeboreshwa ongezeko la uzalishaji wa chakula katika kipindi cha miaka kumi (tani milioni10.94-16.89), lakini upotevu wa chakula baada ya kuvuna imeendelea kuwa changamoto kubwa, upotevu mkubwa ukikadiriwa kuwa asilimia 30-40 kwa mazao yaliyosindikwa na asilimia 50 kwa mazao yasiyosindikwa.

Dkt Tizeba alisema kuwa kutokana na tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na shirika la chakula Duniani wakishirikiana na Rockefeller foundation katika zao la mahindi na nyanya nchini Tanzania, zimeonesha kwamba, katika hatua ya uvunaji, upotevu wa nyanya ni kati ya asilimia 15-25% na mahindi ni kati ya asilimia 6.1-11.6. Na ambao katika hatua ya usafirishaji na uuzaji upotevu ni kati ya 1-8%. Katika utafiti huu ongezeko la upoteaji lilionekana kuwa kati ya 10-23%. Na katika hatua ya hifadhi za muda upotevu umeripotiwa kuwa asilimia 6.2.

Alisema nchi ya Tanzania, kama zilivyo nchi zingine za Afrika, husumbuliwa na matatizo makubwa kadhaa ya uhifadhi chakula ambayo hupelekea upotevu wa rasilimali uzalishaji kama hazitashughulikiwa ipasavyo.

Aliyataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na Teknolojia duni, hasa katika uvunaji na uhifadhi wa chakula baada ya mavuno, Ujuzi hafifu wa mnyororo wa matukio baada ya uvunaji, na Uhaba wa masoko na miundimbinu mibovu, kwani wazalishaji na wanunuzi hawana mawasiliano mazuri kutokana na uhaba wa taarifa na barabara zisizopitika katika misimu yote.

Aidha, matatizo mengine ni pamoja na Uhaba wa fedha katika shughuli mbalimbali baada ya uvunaji, Ushiriki hafifu wa sekta binafsi katika kuwekeza katika mchakato wa shughuli mbalimbali baada ya uvunaji, na katika hatua ya uhifadhi, upotevu hutokana na magonjwa na wadudu ambao husababisha upotevu katika ubora na kiasi.

Aliongeza kuwa upotevu wa chakula baada ya uvunaji umeendelea kuwa tatizo kubwa siyo tu katika chakula lakini pia katika malighafi kwa maendeleo ya viwanda huku akizitaja juhudi zilizofanywa na serekali ya Tanzania kupunguza upotevu wa chakula ambazo ni pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendelea, taasisi za kimataifa kama vile Bill and Melinda Gates foundation, HELVETAS Swiss Inter Cooperation Agency, Rockefeller foundation, AGRA, shirika la chakula duniani, mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yameboresha kwa kiasi kikubwa teknolojia ya uhifadhi kama vile mifuko ya plastiki ya kuhifadhia nafaka ambayo imeonesha kuwa na mafanikio makubwa sana kwa kuzuia wadudu waharibifu kupenya na kushambulia nafaka. 

Hivyo kupunguza matumizi ya madawa ambayo husaidia kulinda afya za walaji na kuongeza kipato cha wazalishaji. Mafunzo kwa wawezeshaji katika mnyororo wa kuongeza thamani, utoaji wa miongozo mbalimbali ya kitaifa ambayo iliwafikia walengwa ilifanywa ili kuongeza maarifa na ujuzi wa uhifadhi baada ya uvunaji.

Njia nyingine za kupunguza upotevu wa chakula nchini Tanzania ni pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo na uhifadhi baada ya mavuno kutoa miongozo ya kitaalamu iliyokuwa na lengo la kupunguza hadi 50% ya upotevu baada ya uvunaji kufikia 2025 kama ilivyobainishwa katika azimio la Malabo na Utekelezaji wa sera ya viwanda ambapo uchakataji wa bidhaa za kilimo umepewa kipaumbele kwa kuongeza thamani kitu ambacho hutegemewa kupunguza upotevu baada ya uvunaji.

Zingine ni Ujengaji wa maghala na vihenge kupitia programu ya matokeo makubwa sasa ili kuongeza uhifadhi na uuzaji wa nafaka, kama vile mahindi na mpunga kwa pamoja. Mradi umezifikia wilaya 12 za nyanda za juu kusini tangu 2013/14. Zaidi ya vijiji 105 vimenufaika na maghala haya na mradi unaendelea na umeshapimwa katika mikoa mingine 6 ya kanda ya kati, mashariki, kaskazini na kanda ya ziwa.

Uanzishaji wa mpango wa miundombinu masoko, uongezaji wa thamani, na uwezeshaji wa kifedha vijijini (2011-2018) unaolenga kupambana na sababu za upotevu wa chakula kwa kuboresha  barabara vijijini, miundombinu ya masoko, na kuanzisha mifuko ya uwezeshaji kifedha katika sekta ya uchakataji wa bidhaa za kilimo. Matokeo ya mradi huu yamepunguza kwa kiasi kikubwa sana upotevu wa chakula, hivyo kuongeza upatikanaji wa chakula nchini.

Pia Kuanzishwa kwa mfumo wa ubadilishanaji bidhaa Tanzania. Kuweka mazao katika masoko yaonekanayo ili kurahisisha uuzaji na kupunguza upoteaji wa bidhaa za kilimo. Chini ya mradi huu mazao yatatunzwa chini ya mfumo vikundi vya wakulima na kuuzwa moja kwa moja  katika mfumo wa kubadilishana mazao

Waziri huyo wa kilimo nchi Tanzania Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba aliuthibitishia mkutano huo uliohudhuriwa na washiriki kutoka nchi zote za Afrika kuwa serikali ya Tanzania ipo tayari katika kuleta maboresho yoyote muhimu kwa kuwawezesha wamiliki wadogo wa mashamba kuwa na vifaa stahiki na maarifa na kuwawezesha kuzalisha mazao bora na kupunguza upotevu wa mazao wakati wa uvunaji, usafirishaji na uhifadhi na kuondokana na zana duni wanazotumia kwenye kilimo.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com