Waziri wa kilimo-Tanzania Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akizungumza juu ya upunguzaji wa upotevu wa chakula wakati wa hotuba yake kwenye mkutano wa Mapinduzi ya kijani Barani Afrika (African Green Revolution Forum-AGRF) unaofanyika kwa siku nne unaofanyika Mjini Kigali nchini Rwanda kuanzia tarehe 5-8 Septemba 2018 mjini Kigali nchini Rwanda. (Picha Na Mathias Canal,WK)
Na Mathias Canal,
Kigali-Rwanda
Imebainika kuwa Barani Afrika, upotevu wa chakula bado ni
changamoto kubwa inayohitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwani zaidi ya
asilimia 30% ya chakula hupotea huku kwa uoande wa mbogamboga na matunda,
upotevu ni wa juu zaidi kwani inakadiriwa kufikia asilimia 50% au zaidi.
Upotevu wa chakula una matokeo hasi katika uhifadhi wa chakula
ambapo ni tatizo la dunia nzima linaloathiri jamii kwa mtu mmoja mmoja na bara
la Afrika kwa ujumla wake. Kutokana na takwimu za Shirika la chakula duniani,
asilimia 30% ya chakula kinachozalishwa kwa matumizi ya binadamu hupotea katika
mchakato wa usambazaji kila mwaka.
Hayo yamebainishwa Jana tarehe 6 Septemba 2018 na
Waziri wa kilimo-Tanzania Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba wakati wa hotuba
yake kuhusu mada juu ya upunguzaji wa upotevu wa chakula kwenye mkutano wa
Mapinduzi ya kijani Afrika (African Green Revolution Forum-AGRF) unaofanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 5-8 Septemba
2018 mjini Kigali nchini Rwanda.
Alisema kuwa hali hiyo inamaanisha makadirio ya Tani bilioni 1.3
ya chakula hayamfikii mlaji wa mwisho. Upotevu huu wa mazao hujumuisha upotevu
wa rasilimali za uzalishaji, kama vile ardhi, maji, nishati na hatimae upotevu
wa kipato kwa watu wote katika mnyororo wa uzalishaji na usambazaji.
Dkt Tizeba alisema kuwa nchini Tanzania, pamoja na kuwa
kumeboreshwa ongezeko la uzalishaji wa chakula katika kipindi cha miaka kumi
(tani milioni10.94-16.89), lakini upotevu wa chakula baada ya kuvuna imeendelea
kuwa changamoto kubwa, upotevu mkubwa ukikadiriwa kuwa asilimia 30-40 kwa mazao
yaliyosindikwa na asilimia 50 kwa mazao yasiyosindikwa.
Dkt Tizeba alisema kuwa kutokana na tafiti za hivi karibuni
zilizofanywa na shirika la chakula Duniani wakishirikiana na Rockefeller
foundation katika zao la mahindi na nyanya nchini Tanzania, zimeonesha kwamba,
katika hatua ya uvunaji, upotevu wa nyanya ni kati ya asilimia 15-25% na
mahindi ni kati ya asilimia 6.1-11.6. Na ambao katika hatua ya usafirishaji na
uuzaji upotevu ni kati ya 1-8%. Katika utafiti huu ongezeko la upoteaji
lilionekana kuwa kati ya 10-23%. Na katika hatua ya hifadhi za muda upotevu
umeripotiwa kuwa asilimia 6.2.
Alisema nchi ya Tanzania, kama zilivyo nchi zingine za Afrika,
husumbuliwa na matatizo makubwa kadhaa ya uhifadhi chakula ambayo hupelekea
upotevu wa rasilimali uzalishaji kama hazitashughulikiwa ipasavyo.
Aliyataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na Teknolojia duni, hasa
katika uvunaji na uhifadhi wa chakula baada ya mavuno, Ujuzi hafifu wa mnyororo
wa matukio baada ya uvunaji, na Uhaba wa masoko na miundimbinu mibovu, kwani
wazalishaji na wanunuzi hawana mawasiliano mazuri kutokana na uhaba wa taarifa
na barabara zisizopitika katika misimu yote.
Aidha, matatizo mengine ni pamoja na Uhaba wa fedha katika
shughuli mbalimbali baada ya uvunaji, Ushiriki hafifu wa sekta binafsi katika kuwekeza
katika mchakato wa shughuli mbalimbali baada ya uvunaji, na katika hatua ya
uhifadhi, upotevu hutokana na magonjwa na wadudu ambao husababisha upotevu
katika ubora na kiasi.
Aliongeza kuwa upotevu wa chakula baada ya uvunaji umeendelea
kuwa tatizo kubwa siyo tu katika chakula lakini pia katika malighafi kwa
maendeleo ya viwanda huku akizitaja juhudi zilizofanywa na serekali ya Tanzania
kupunguza upotevu wa chakula ambazo ni pamoja na kushirikiana na wadau
mbalimbali wa maendelea, taasisi za kimataifa kama vile Bill and Melinda Gates
foundation, HELVETAS Swiss Inter Cooperation Agency, Rockefeller foundation,
AGRA, shirika la chakula duniani, mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo
yameboresha kwa kiasi kikubwa teknolojia ya uhifadhi kama vile mifuko ya
plastiki ya kuhifadhia nafaka ambayo imeonesha kuwa na mafanikio makubwa sana
kwa kuzuia wadudu waharibifu kupenya na kushambulia nafaka.
Hivyo kupunguza matumizi ya madawa ambayo husaidia kulinda afya
za walaji na kuongeza kipato cha wazalishaji. Mafunzo kwa wawezeshaji katika
mnyororo wa kuongeza thamani, utoaji wa miongozo mbalimbali ya kitaifa ambayo
iliwafikia walengwa ilifanywa ili kuongeza maarifa na ujuzi wa uhifadhi baada
ya uvunaji.
Njia nyingine za kupunguza upotevu wa chakula nchini Tanzania ni
pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo na uhifadhi baada ya
mavuno kutoa miongozo ya kitaalamu iliyokuwa na lengo la kupunguza hadi 50% ya
upotevu baada ya uvunaji kufikia 2025 kama ilivyobainishwa katika azimio la
Malabo na Utekelezaji wa sera ya viwanda ambapo uchakataji wa bidhaa za kilimo
umepewa kipaumbele kwa kuongeza thamani kitu ambacho hutegemewa kupunguza
upotevu baada ya uvunaji.
Zingine ni Ujengaji wa maghala na vihenge kupitia programu ya
matokeo makubwa sasa ili kuongeza uhifadhi na uuzaji wa nafaka, kama vile
mahindi na mpunga kwa pamoja. Mradi umezifikia wilaya 12 za nyanda za juu
kusini tangu 2013/14. Zaidi ya vijiji 105 vimenufaika na maghala haya na mradi
unaendelea na umeshapimwa katika mikoa mingine 6 ya kanda ya kati, mashariki,
kaskazini na kanda ya ziwa.
Uanzishaji wa mpango wa miundombinu masoko, uongezaji wa
thamani, na uwezeshaji wa kifedha vijijini (2011-2018) unaolenga kupambana na
sababu za upotevu wa chakula kwa kuboresha barabara vijijini, miundombinu
ya masoko, na kuanzisha mifuko ya uwezeshaji kifedha katika sekta ya uchakataji
wa bidhaa za kilimo. Matokeo ya mradi huu yamepunguza kwa kiasi kikubwa sana
upotevu wa chakula, hivyo kuongeza upatikanaji wa chakula nchini.
Pia Kuanzishwa kwa mfumo wa ubadilishanaji bidhaa Tanzania.
Kuweka mazao katika masoko yaonekanayo ili kurahisisha uuzaji na kupunguza
upoteaji wa bidhaa za kilimo. Chini ya mradi huu mazao yatatunzwa chini ya
mfumo vikundi vya wakulima na kuuzwa moja kwa moja katika mfumo wa
kubadilishana mazao
Waziri huyo wa kilimo nchi Tanzania Mhe Mhandisi Dkt Charles
Tizeba aliuthibitishia mkutano huo uliohudhuriwa na washiriki kutoka nchi zote
za Afrika kuwa serikali ya Tanzania ipo tayari katika kuleta maboresho yoyote
muhimu kwa kuwawezesha wamiliki wadogo wa mashamba kuwa na vifaa stahiki na
maarifa na kuwawezesha kuzalisha mazao bora na kupunguza upotevu wa mazao
wakati wa uvunaji, usafirishaji na uhifadhi na kuondokana na zana duni
wanazotumia kwenye kilimo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment