Na Asteria Muhozya, Simanjiro
Waziri wa Madini Angellah Kairuki
amesema Serikali itaaendelea kusimamia
ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na watakaokwenda kinyume na matakwa ya Sheria, kiama chao kinakuja.
Waziri Kairuki
aliyasema hayo tarehe 1 Agosti wakati wa ziara yake mkoani Manyara wakati
alipotembelea migodi mbalimbali ya madini
ya tanzanite ndani ya ukuta wa Mirerani.
Alisema ziara hiyo
ililenga kuangalia suala zima la ulinzi katika ukuta unaozunguka migodi
ya tanzanite, shughuli za uchimbaji madini mengine zinavyofanyika na
kuangalia namna uzalishaji wa madini ya tanzanite unavyoendelea katika
migodi husika.
Kairuki aliongeza
kuwa, ziara hiyo ililenga kuangalia
namna Sheria ya Madini inavyotekelezwa, masuala ya Mikataba ya watumishi katika
migodi na namna migodi husika inavyolipa
kodi mbalimbali za Serikali yakiwemo masuala ya usalama sehemu za kazi
na wafanyakazi kwa ujumla.
“Utoroshaji madini
hausaidii, fedha ni za haraka lakini zinawaadhibu watanzania walio wengi kwa
kuwa, fedha hizo hizo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo.
Hivyo, kila mtanzania awe mlizi wa mwenzake,” alisema Kairuki.
Awali,
akizungumza katika eneo Lemshuku
kunakofanyika shughuli za uchimbaji wa madini ya Green Garnet, waziri Kairuki
alisema kuwa, serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo katika kuchangia
pato la taifa kupitia shughuli za uchimbaji, hivyo akawaasa wachimbaji nchini
kufuata Sheria, kanuni na taratibu ili kufanya shughuli halali ikiwemo kulipa
kodi stahiki.
Akizungmzia suala la
ruzuku kwa wachimbaji wadogo, waziri Kairuki alisema hivi sasa serikali
imesitisha kwa muda utoaji rukuzu kwa kuwa inaandaa utaratibu wa wazi na
endelevu ambao utawezesha wachimbaji na
serikali kunufaika kupitia rasilimali madini.
Aliongeza kuwa, serikali
inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa shughuli za uchimbaji mdogo wa madini
ikiwemo kuhakikisha kuwa inawawezesha wachimbaji kutoka uchimbaji mdogo kwenda
katika uchimbaji wa kati na kuongeza, “ tayari tumetenga maeneo zaidi ya 44 kwa
ajili ya wachimbaji wadogo.
Akitolea ufafanuzi
suala la vibarua katika migodi ya madini, aliwataka wale wote wanaofanya
vibarua katika maeneo hayo kuhakikisha kuwa, wanapata mikataba yao kabla ya
kuanza kazi.
Kuhusu masuala ya
utoaji leseni za uchimbaji madini, Waziri Kairuki alisema
ndani ya kipindi cha wiki 2 Tume ya Madini itaanza kutoa leseni kwa
waombaji waliokidhi vigezo na kuongeza kuwa, kwa wanaomiliki leseni bila
kuziendeleza watanyang’nywa na hivyo akawaasa wamiliki wasiokuwa na uwezo wa
kuendeleza maeneo yao kutoa tarifa ili waweze kuunganishwa na wenye uwezo wa
kuwekeza waweze kushirikiana.
Pia, waziri Kairuki
alihamasisha kuhusu uwekezaji katika mashine za kukata na kunga’risha madini
ili kuwezesha shughuli hizo kufanyika nchini na kuongeza kuwa, kupitia Sheria
Mpya ya Madini hairuhusu yoyote kusafirisha
madini ghafi nje ya nchi.
Kwa upande
wake, Kamishna wa Madini, Mhandisi David
Mlabwa, alisema ni lazima Sheria, Kanuni
na taratibu zizingatiwe wakati wa utekelezaji shughuli za uchimbaji madini na
kuongeza kuwa, serikali inatambua mchango wa kila aina ya madini yanayopatikana
nchini.
Naye, Kaimu Mkuu wa
Wilaya ya Simanjiro, Tumaini Magesa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto alisema
kuwa, shughuli za uchimbaji katika eneo la Mirerani zinaendelea na hivyo
serikali itaendelea kuboresha ulinzi na kuhakikisha kwamba unaimalika.
0 comments:
Post a Comment