METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 16, 2018

WAZIRI MKUU AMPA HEKO DKT TIZEBA USIMAMIZI WENYE TIJA KWENYE KOROSHO, AMTAKA KUIPAISHA NA TUMBAKU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) akilakiwa na mwenyeji wake Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba (Mb) mara baaada ya kuwasili kijijini Kangeme Kata ya Ulowa kukagua ghala la tumbaku la Chama cha msingi Kangeme. Jana 16 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maeleazo kutoka kwa  Waziri  wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba. (kushoto) wakati alipokagua uuzaji wa tumbaku katika Chama  cha Ushirika cha Msingi cha Kangeme katika Halmashauri ya  Ushetu, Julai 16, 2018.  Kulia kwake  ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Nchini, Dkt Titus Kamani, Jana 16 Julai 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata akimshuhudia Waziri  wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba (katikati) akijaribu kuendesha pikipiki moja kati ya tatu alizomkabidhi kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo Halmashauri ya Ushetu, Julai 16, 2018. Katika hafla hiyo pia Waziri Mkuu alimkabidhi Dkt Tizeba gari aina ya Toyota Land Cruiser. Mwingine pichani ni Waziri wa afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mhe Ummy Mwalimu (Mb) na Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEM) Mhe Joseph Kakunda.

Na Mathias Canal, Ushetu-Shinyanga

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) amempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba katika kipindi cha miaka miwili tangu ateuliwe kuhudumu katika nafasi hiyo kwa kupaisha zao la Korosho kutoka shilingi 1470 kwa kilo moja au 1480 na hatimaye kufikia shilingi 4300 kwa kilo moja.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita zao hilo lilikuwa likiuzwa kati ya shilingi 700 mpaka 800 kwa kila kilo moja jambo ambalo lilimdidimiza mkulima kwani aliwekeza nguvu nyingi katika Kilimo lakini tija ya nguvu zake ilikuwa na thamani ndogo.

Waziri Mkuu alitoa pongezi hizo jana 16 Julai 2018 kijijini Kangeme Kata ya Ulowa wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya.

Alitoa pongezi hizo pia kwa waziri Tizeba kutokana na juhudi zake anazozifanya ikiwa ni pamoja na kuongezeka maradufu kwa bei kwenye zao la ufuta kutoka shilingi 1000 kwa kilo hadi kufikia 3000 kwa kilo.

Aidha, katika kuongeza ufanisi kwenye kuimarisha na kufanua mabadiliko ya kimazoea katika vyama vya msingi, Waziri Mkuu alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule kuwakamata viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa upotevu wa dola za marekani 21,000 za chama hicho.

"Wabebe hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko wapi na jambo la kwanza wailete hiyo fedha ya wakulima. Wakishindwa kurejesha fedha, wawekwe ndani," alisema.

Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kuwaita viongozi wa chama cha Mkombozi watoke hadharani na kubaini kuwa hakuwepo hata mmoja. Inadaiwa kwamba walitoroka baada ya wananchi kuanza kuzomea.

Kamanda Haule amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwenyekiti, Bw. Shilinde Abdallah na mhasibu wa AMCOS hiyo, Bw. Kulwa Shinzi pamoja na wajumbe saba wa bodi ya chama hicho.

Akizungumzia kuhusu Ushirika, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kufufua ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima. "Tumeamua kurudisha ushirika aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo kwa viongozi waliopata dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda kupata ulaji.”

“Tunataka ushirika unaosimamiwa na viongozi waaminifu. Kwenye ushirika kuna fedha na kuna mali za chama, kwa hiyo ni lazima tupate viongozi ambao ni waaminifu,” alisema.

Waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba alisema kuna tatizo katika uteuzi (grading) wa tumbaku kwani wakulima wanalima tumbaku nzuri lakini katika upangaji bei, wanalipwa bei ndogo. “Kuna wakulima wanakidai chama cha Mkombozi kiasi cha dola za Marekani ambayo ni madai ya tumbaku waliyoiuza tangu mwaka 2014.”

Akizungumzia kuhusu Ushika Afya, Dkt Tizeba aliongeza kuwa Tume ya maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wameunda mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya Ushirika nchini ikiwa ni mafanikio yanayoendelea kuonekana katika kuimarisha Ushirika nchini kwa kuakisi utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo mkataba kati ya wananchi na serikali katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020.

Alisema kupitia utaratibu huo wanachama Wa Ushirika Afya atanufaika na huduma za afya zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya zaidi ya elfu sita na miatano (6500) vilivyosajiliwa na Mfuko Wa Taifa Wa Bima ya Afya nchini na hatimaye kuchangia kikamilifu katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa nchi.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com