METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, July 12, 2018

WANANCHI WAHAMASISHWA KUIMARISHA ULINZI





Wananchi wamehamasishwa kuimarisha ulinzi ili kujilinda wao wenyewe na mali zao dhidi ya watu wenye nia ovu

Hayo yamesemwa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa muendelezo wa ziara yake katika kata za Kahama na Shibula juu ya kukagua miradi inayotekelezwa ndani ya jimbo hilo, kusikiliza kero na changamoto, kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kuzungumza na watumishi wa umma, wastaafu, viongozi wa dini, viongozi wa mitaa na wazee maarufu ambapo amewahamasisha wananchi wa kata hizo kuhakikisha wanashiriki katika kutekeleza wajibu wao wa kujilinda na kulinda mali zao dhidi ya watu wenye nia ovu badala ya kuachia jeshi la polisi peke yake kitendo ambacho kinachangia kutokea kwa matukio ya kihalifu maeneo tofauti tofauti ya jimbo hilo

‘… Kulikuwa na utaratibu wa kujilinda kupitia mitaa yetu suala hili limeishia wapi?, Kwasababu wewe ukilala ndani unastarehe ukafikiri askari nane watalinda watu laki mbili ni ngumu …’ Alisema

Aidha Dkt Mabula amewaasa wananchi hao kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa sahihi za vitendo vya kihalifu vinavyofanyika ndani ya maeneo yao na kuwafichua watu wote wanaoonekana kuwa na nia ovu ya kutekeleza matukio hayo kwani jukumu la kulinda usalama wa raia na nchi kwa ujumla ni jukumu la kila mtu na si serikali peke yake kama inavyoelekeza katiba ya nchi ya Tanzania.

Mhe Mabula pia amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati huku akisisitiza kuwa hatavumilia uzembe wowote utakaosababisha kukwama kwa miradi hiyo sambamba na kuwaomba wananchi wa kata ya Kahama kuhakikisha wanatumia nafasi za ajira zinazojitokeza kupitia utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo.

Kwa upande wake afisa mipango miji wa manispaa ya Ilemela ndugu Kennedy Chigulu akijibu hoja zilizojitokeza kutoka kwa wananchi kupitia ziara hiyo amewataka wananchi kuhakikisha hawajengi kiholela kwa kufuata sheria na taratibu za mipango miji ikiwa ni pamoja na kutovamia maeneo ya jeshi kutokana na sababu za usalama wa nchi huku akiwahakikishia kuwa manispaa ya Ilemela kupitia wizara ya ardhi imeendelea kutatua kero za ardhi wakati wizara ya ulinzi ikijipanga kulipa fidia kwa maeneo yote stahiki iliyoyatwaa na hivyo kuwa wavumilivu wakati madai yao yakifanyiwa kazi.

Ziara hiyo iliongozwa na mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama ambae pia ni Kaimu mkuu wa wilaya ya Ilemela Mwl. Khadija Nyembo na kuhudhuriwa na watalaamu wote wa manispaa ya Ilemela wakiongozwa na Mstahiki Meya wa manispaa Ilemela Mhe Renatus Mulunga, Kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo ndugu Daniel Batare, Katibu siasa na uenezi wa CCM wilaya ya Ilemela na diwani wa kata ya Kahama.

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
10.07.2018
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com