METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 16, 2018

DKT TIZEBA AAGIZA TIMU YA UCHUNGUZI ZAO LA TUMBAKU KUTUA USHETU

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akitoa salamu za Wizara yake mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya uliofanyika kijijini Kangeme Kata ya Ulowa, Leo 16 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maeleazo kutoka kwa  Waziri  wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba. (kushoto) wakati alipokagua uuzaji wa tumbaku katika Chama  cha Ushirika cha Msingi cha Kangeme katika Halmashauri ya  Ushetu, Julai 16, 2018.  Kulia kwake  ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeloeo ya Ushirika Nchini, Dkt. Titus Kamani.
Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Ushetu Mkoani shinyanga wakimsikiliza kwa makini waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba (Mb) wakati akitoa salamu za wizara yake kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya uliofanyika kijijini Kangeme Kata ya Ulowa, Leo 16 Julai 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Fao la Ushirika Afya ambalo litawawezesha wanaushirika kunufaika na huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwenye kijiji cha Kangeme katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga Julai 16, 2018.  Kushoto kwake ni  Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba, watatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akitoa salamu za Wizara yake mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya uliofanyika kijijini Kangeme Kata ya Ulowa, Leo 16 Julai 2018.

Na Mathias Canal-WK, Ushetu-Shinyanga
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ameagiza timu ya uchunguzi kuzuru katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga ili kubaini changamoto za uuzaji wa zao la Tumbaku.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo Leo 16 Julai 2018 kijijini Kangeme Kata ya Ulowa wakati akitoa salamu za Wizara ya Kilimo mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya.

"Mhe Waziri Mkuu nimewahi kutembea katika masoko mengi ya Tumbaku lakini sikuwahi kufika mahala tukawaona wananchi wananung'unika kama walivyofanya wananchi wa hapa maana yake moja tu kwamba kuna jambo halipo sawa hapa, tumbaku hailimwi Ushetu peke yake inalimwa katika maeneo mengi nchini lakini nilichokiona hapa kinanitia wasiwasi" 

"Inaelekea Mhe Waziri Mkuu katika uteuzi wa Tumbaku kuna kasoro ambapo wakulima wamelima Tumbaku nzuri lakini inapokuja kuteuliwa inapangiwa madaraja ya chini hivyo inaonekana kama Tumbaku yao haina Ubora" Alikaririwa Dkt Tizeba

Alisema kuwa timu hiyo ya uchunguzi itakuwa na jukumu la kufuatilia na kubaini kuwa Uteuzi uliofanyika ulikuwa wa haki ama vinginevyo na bei ya Tumbaku waliyopewa wananchi sio ya kutengenezwa bali inatokana na madaraja waliyozalisha.

Dkt Tizeba alikielekeza Chama cha msingi cha wakulima Mkombozi ambacho bado hakijawalipa wakulima kiasi cha Dola 21,000 katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2014 mpaka sasa kuhakikisha msimu huu kiasi hicho cha fedha kinalipwa kwa wananchi kutoka kwenye makato ya chama chenyewe.

Alisisitiza kuwa atafatilia kwa karibu jambo hilo ili kuhakikisha kwamba haki ya wananchi inapatikana mwaka huu kwani mambo kama hayo ndiyo yanayopelekea wananchi kulalamika wakitaka majawabu kamili.

Alisema, wananchi kuendelea kulima Tumbaku kwa mikono kunazidi kuwafanya wakulima kuwa tegemezi wa makampuni kwani kila mwaka wanakopa na kuingizwa katika mkataba ambapo wakishaingizwa kwenye mkataba huo wafanyabiashara wengine hawawezi kuja kununua.

Alisema kupitia mikataba hiyo Tumbaku ya wakulima haiingii katika ushindani  kama ilivyo katika Mazao mengine kama vile korosho na ufuta yanavyoshindaniwa na wanunuzi hivyo kupelekea bei kupanda na kuongeza kipato kwa wakulima.

"Sasa sisi wakulima tumejifunga katika mikopo na katika kukopa tunakuwa na mtoa mikopo mmoja ambaye ni Benki ambazo zinataka kuingia mkataba na makampuni na kuwapa makadirio badae wanakuja mwenyewe kununua hapo bei itapanda namna gani...? kwa hivyo dawa ni moja tu wananchi kujifunza kujitegemea kwa kuweka akiba kwa ajili ya uwezalishaji wa mwaka unaofuata" Alisema Dkt Tizeba

Aliwasihi wananchi hao endapo wataridhia kuwekwa utaratibu kwa mauzo ya mwaka huu ili msimu wa mwaka 2019 kuwe na utaratibu wa wakulima kujigharamia wenyewe pembejeo bila kuingia kwenye mikopo ambayo ina riba kubwa ya asilimia 18% mpaka asilimia 20%.

Alisema kuwa mbinu mojawapo ya kupandisha tija ya bei kwenye zao hilo la Kahawa ni kuongeza wanunuzi kufikia walau watano kwani kuwa na mnunuzi mmoja tija itaendelea kuwa ndogo huku wakulima wakiendelea kunyonywa.

Alisema kuwa msimu wa zao la Pamba utakapofika hakutakuwa na makato wananchi watagaiwa mbegu, dawa na mabomba ya kupulizia dawa pasina malipo.

Akizungumzia kuhusu Ushika Afya, Dkt Tizeba aliongeza kuwa Tume ya maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wameunda mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya Ushirika nchini ikiwa ni mafanikio yanayoendelea kuonekana katika kuimarisha Ushirika nchini kwa kuakisi utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo mkataba kati ya wananchi na serikali katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020.

Alisema Ofisi ya Mrajis na Mfuko wa Bima ya Afya unaendelea na uhamasishaji kwa wanachama wa vyama vya Ushirika na wakulima ili waweze kujiunga kwenye utaratibu wa matibabu kupitia Ushirika Afya kwenye mikoa inayolima Korosho, Pamba, Tumbaku, Chai na Kahawa.

Katika hafla hiyo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa amemkabidhi Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba gari moja aina ya Toyota Land Cruiser kwa ajili ya idara ya kilimo katika Halmashauri ya Ushetu sambamba na pikipiki tatu zilizonunuliwa kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya maafisa ugani ili kuongeza ufanisi na tija katika ukuzaji wa sekta ya Kilimo katika Wilaya hiyo.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com