METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 16, 2018

Biteko akamata Shehena ya sampuli za madini yaliyotelekezwa Ruvuma

Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko (kulia) akijionea sampuli ya mwamba wa madini. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya Songea Mhe. Pololet Mgema. Jana 16 Julai 2018.
Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko (kulia) akikagua mkataba wa upangaji baina ya wamiliki wa sampuli hizo na mwenye nyumba. Jana 16 Julai 2018.
Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mtepa Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma na kuwapongeza kwa kushirikiana na serikali katika kufichua vitendo viovu katika jamii. Jana 16 Julai 2018.
Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko (kushoto) alifanya mazungumzo mafupi na Mkuu wa Mkoa Ruvuma Mhe Christina Mndeme (katikati). Kulia ni Katibu Tawala mkoani Ruvuma, Hassan Bendeyeko.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM mkoani Ruvuma Ndg Amina Imbo (kulia) akizungumza jambo baada ya Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko (kushoto) kufika katika ofisi za chama hicho.
Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mkoani Ruvuma akiwemo Mkuu wa Wilaya Songea Mhe.Pololet Mgema (wa pili kulia), Mbunge Jimbo la Madaba Mhe.Joseph Mhagama (wa pili kushoto) pamoja na Katibu wa CCM mkoa Ruvuma Ndg.Amina Imbo ( wa tatu kushoto).

Na George Binagi, Ruvuma

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameshitushwa na shehena kubwa ya madini ya aina mbalimbali iliyotelekezwa katika Kijiji cha Mtepa,  Halmashauri ya Madaba, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma na kuagiza shehena hiyo kufanyiwa uchunguzi ili kubaini aina ya madini yaliyomo.

Mhe Biteko ambaye aliwasili jana Julai 16, 2018 mkoani Ruvuma kwa ajili ya ziara ya kikazi, alipata taarifa toka kwa raia mwema ya kuhifadhiwa kwa shehena hiyo nyumbani kwa mzee Allan Mbilinyi ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho tangu mwaka 2014 huku wahusika wakitokomea kusikojulikana.

Alisema kitendo cha kuhifadhi sampuli za madini hayo nyumbani ni kinyume cha sheria ya madini ambayo inataka sampuli za aina hiyo kupelekwa katika ofisi ya Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).

Aidha alieleza kanuni za sheria za madini kifungu Cha 23 kinataka kila mwenye sampuli, ama taarifa ama kingine chochote kikiwa na uhusiano na madini ndani ya siku 30 awasilishe taarifa hizo kwa GST tangu tarehe ya kuchapishwa kwa kanuni hizo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe Pololet Mgema alionya kwamba wote wanaohusika na shehena hiyo lazima watafutwe ili waeleze walipoitoa na kwa nini wameitelekeza kijijini hapo kwa muda mrefu na kwamba kama kuna kiongozi yeyote alihusika na sampuli hizo lazima achukuliwe hatua za kisheria kwani haiwezekani sampuli za madini kukaa miaka minne bila viongozi ngazi ya Wilaya na Halmashauri kuwa na taarifa.

Awali Mzee Allan Mbilinyi ambaye shehena hiyo imehifadhiwa nyumbani kwake alisema mkataba wa upangishaji unaonyesha kuna jumla ya makasha 209 na wamiliki wakiwa ni kampuni ya kichina ya Sinohydro.

“Mimi sikuwepo nyumbani na niliporudi nilikuta mke wangu ameingia mkataba wa upangaji na wenye haya madini wa shilingi laki moja na elfu themanini kwa mwaka. Lakini nikasema mbona bei hii hailipi hivyo nikataka waongeze malipo, lakini kila nikiwatafuta siwapati”. Alieleza mzee Mbilinyi na kuongeza kwamba huenda sampuli za madini hayo zimetelekezwa baada ya serikali kuzuia usafirishaji makinikia nje ya nchi.

Nao wananchi wa kijijini hapo walieleza kuwa hiyo ni sehemu ndogo tu ya shehena ambayo wachina walikua wakisomba.

“Mzigo uliochukuliwa ni mkubwa mno huo uliofichwa ndani ni kiasi kidogo tu. Na naona waliukimbia Baada ya Rais Magufuli kubana madini” alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.

MWISHO.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com