METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 7, 2018

MABULA ATAKA HALMASHAURI KUTENGA MAENEO YA UJENZI WA NYUMBA ZA WATUMISHI




Na Munir Shemweta, Nachingwea

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula ameziataka Halmashauri nchini kutenga maeneo ya ujenzi wa nyumba za watumishi yenye miundombinu ili shirika la nyumba la taifa (NHC) liweze kujenga nyumba za gharama nafuu.

Mhe Mabula amesema hayo jana wilayani Nachingwea mkoa wa Lindi wakati wa ziara yake mkoani Lindi kukagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi pamoja na kuhamasisha ulipaji kodi za ardhi kwa wananchi wa mikoa ya lindi na Ruvuma.

Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa halitakiwi kuingia gharama ya kutafuta maeneo pamoja na kuweka miundombinu kwani kwa kufanya hivyo kutalilazimu shirika kujenga nyumba na kuziuza kwa gharama kubwa jambo litakalowafanya watumishi na watu wengine wanaozihitaji kushindwa kuzinunua au kupanga.

‘’NHC haitakiwi kuingia ghrama zozote, halmashauri ndiyo inapaswa kutenga maeneo na kuhakikisha huduma zote muhimu kama maji, barabara, umeme vinakuwepo na Shirika kazi yake iwe kujenga nyumba tu’’ alisema Mabula

Alibainisha kuwa, iwapo halmashauri zitatenga maeneo na kupeleka huduma zote muhimu basi shirika la nyumba litaweza kujenga nyumba kwa gharama ndogo na kuziwezesha halmahauri kuwa na nyumba zake ambazo zinaweza kuuzwa au kuwapangishwa na kubaki kama rasilimali ya Halmashauri.

Amelitaka shirika la nyumba la Taifa kuhakikisha linaingia makubaliano ya ujenzi wa nyumba na halmashauri kwanza kabla ya kuanza ujenzi ili kuepuka kujenga nyumba zitakazokosa mnunuzi kama ilivyojitokeza kwa baadhi ya maeneo jambo linalolipa hasara shirika la nyumba.

‘’kuna maeneo halmashauri zimejengewa nyumba na shirika lakini hazijauzwa sasa utawezaje kujenga nyingine wakati ulizojenga awali hazijauzwa? ‘’ alihoji Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mabula ameisifu halmashauri ya Uyui kwa kujengewa nyumba na Shirika la Nyumba la Taifa na kuzinunua zote 32  ilizojengewa  jambo alilolielezea kuwa ni mfano wa kuigwa na halmashauri nyingine.

Kwa mujibu wa Mabula, malengo ya shirika katika ujenzi wa nyumba ni kuuza, kupangisha na kuwa na mpangaji mnunuzi jambo alilolieleza kuwa linalisaidia shirika kupata fedha za kujiendesha na wakati huo kuwezesha wananchi kuwa na makazi bora.

Kwa upande wake, meneja wa shirika la nyumba la taifa mkoa wa Lindi Gibson Mwaigomole amesema shirika lake limekuwa likizungumza na halmshauri za mkoa huo lengo likiwa kuhakikisha wanajenga nyumba kwa ajili ya kuziuza kwa halmashauri.

Hata hivyo, Alisema baadhi ya halmashauri zimekuwa na uhitaji wa nyumba na na tayari wamezungumza nazo na kutolea mfano wa Halmashauri ya manispaa ya Lindi kuwa ni moja ya halmashauri za mkoa wa Lindi iliyoomba kujengewa 54.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com