Waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akishiriki uvunaji wa zao la Pamba, wakati alipotembelea Kijiji cha Mwakipoleja kilichopo kata ya Mbutu Wilayani Igunga Mkoani Tabora, Juzi 17 Juni 2018. Picha zote Na Mathias Canal-WK
Waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akimkabidhi Felista Elius pamba aliyovuna, wakati alipotembelea Kijiji cha Bukama kilichopo kata ya Mbutu Wilayani Igunga Mkoani Tabora, Juzi 17 Juni 2018.
Na Mathias Canal-WK, Igunga-Tabora
Waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba ameshtushwa na wanawake
pekee kuwa kwenye mashamba wakivuna pamba ilihali waume zao wakiwa kwenye Chang’aa
(Pombe za kienyeji) ama kwenye vijiwe kupiga soga.
Dkt Tizeba ameshtushwa na wanawake wengi kuwa shambani wakivuna
pamba ilihali waume zao wakiwa kwenye vijiwe vya pombe za kienyeji mara baada
ya juzi 18 Juni 2018 kutembelea katika Kijiji cha Bukama na Mwakipoleja
vilivyopo katika kata ya Mbutu Wilayani Igunga Mkoa wa Tabora kujionea hali ya
mavuno ya zao la pamba.
Waziri wa Kilimo Mhe Tizeba amesema kuwa kwa muda mrefu imekuwa
kama utamaduni wa kawaida kwa wanaume katika maeneo mengi nchi kuwatelekeza
wake zao wakati wa kuvuna pamba lakini wakati wa mauzo wanawake hao huachwa
nyumbani pasina kujua kiasi kilichopatikana baada ya mauzo.
Hata hivyo wananchi wengi ambao ni wakulima wa pamba kijijini
hapo wameishukuru Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa zao hilo,
ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada inayosimamiwa na Vyama vya
Msingi vya Ushirika (AMCOS).
Pia wakulima hao wameiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na
maghala makubwa na ya kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni kuhakikisha
pamba inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya isipoteze ubora.
Mkulima wa pamba Ndg Elius
Bushia kutoka kijiji cha Bukama alimueleza waziri wa kilimo kuwa awali kabla
pamba kuanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora lilikuwa halizingatiwi na
wakulima wengi kwani pamba yake ikikataliwa na kampuni moja alikuwa
na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine hivyo jambo hilo lilichangia
kupunguza ama kuisha thamani ya zao hilo.
Hata hivyo ameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa
Ushirika ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na pia isaidie kutoa
elimu kwa wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima wengi waweze
kujiunga.
Dkt Tizeba aliwaahidi wananchi hao kuwa changamoto
zilizojitokeza kwenye kilimo mwaka huu serikali itazifanyia kazi ili
kuzipunguza au kuzitokomeza kabisa huku akiwatangazia neema wakulima hao kuwa
serikali itatoa mbegu na dawa za pamba bure ili wakulima wanufaike na matunda
ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe Dkt. John Pombe Magufuli.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment