Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitoa heshima za mwisho kwa mfanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Marehemu Atufigegwe Mwakasege, nyumbani kwa marehemu eneo la Kikuyu mjini Dodoma Aprili 25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaleo (Jumatano, Aprili, 25, 2018) ameshiriki maziko ya aliyekuwa mtumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu marehemu Bw. Atufigwege Mwakasege yaliyofanyika katika makaburi ya Kikuyu mjini Dodoma.
Bw. Mwakasege ambaye alihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu Februari 29, 2016 akitokea Ofisi ya Rais-TAMISEMI amefariki dunia Aprili 23 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa amelazwa baada ya kuugua.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama amesema kifo hicho kimeiachia pengo kubwa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na familia.
“Natumia fursa hii kutoa pole kwa wanafamilia hususan mjane na watoto. Marehemu ameacha pengo ndani ya familia, hivyo tumuombe Mwenyezi Mungu awape uwezo na nguvu ya kuweza kuhimili pengo hilo.”
Marehemu Bw. Mwakasege ambaye alizaliwa Desemba 25, 1959 katika kitongoji cha Mwanjelwa mkoani Mbeya, ameacha mjane Bibi Judith Mwakasege pamoja na watoto wane ambao ni Henry, Joel, Eva na Kelvin Mwakasege.
Maziko hayo pia yamehudhuriwa na Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mama Mary Majaliwa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Profesa Faustine Kamuzola, Katibu Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge) Bi. Maimuna Tarishi, Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE, APRILI 25, 2018.
0 comments:
Post a Comment