WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amekemea uharibifu
wa
makusudi wa miundombinu ya barabara na majengo unaofanywa na baadhi ya
wananchi na kuwataka waache tabia hiyo mara moja.
Ametoa kauli hiyo leo
asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa
Magu, Bw. Kiswaga Destery aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani dhidi ya
wananchi wanaoharibu miundombinu ili wakauze kama vyuma chakavu kwa vile
Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu hiyo.
Waziri Mkuu amesema
Serikali inatumia fedha nyingi sana kuboresha miundombinu mbalimbali nchini na
kwamba kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda miundombinu hiyo.
“Serikali inatumia
fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara na majengo ili kutolea huduma,
Watanzania wote tunao wajibu wa kuilinda na endapo itatokea mtu anaihujumu
miundombinu hii, Serikali hatuwezi kukaa kimya, lazima tutachukua hatua,”
ameonya.
Amesema jukumu la
ulinzi ni la Watanzania wote, na kila Mtanzania anayo dhamana ya ulinzi na
usalama wa ndani ya nchi ikiwemo kuilinda miundombinu. “Juzi niliona kwenye
televisheni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mheshimiwa
Jaffo akishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Shinyanga, wamekamata
Fuso lililojazwa vyuma vilivyong’olewa kwenye barabara, ni vile ambavyo
vinawekwa kwenye daraja na kingo za barabara,” amesema.
“Huu ni uharibifu
ambao hatuwezi kuvumilia, na katika hili Watanzania lazima tuungane pamoja
tukemee tabia hii. Tunatumia fedha nyingi kujenga kingo za barabara, kuashiria
maeneo yenye hatari lakini Watanzania wengine wanakuja kung’oa kwa matumizi
yao. Mimi naamini Mkoa wa Shinyanga utakuwa umechukua hatua kali dhidi yao,”
amesema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193
- DODOMA.
ALHAMISI, MEI 17,
2018.
0 comments:
Post a Comment