METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, May 18, 2018

SERIKALI IPO MAKINI NA AJIRA ZA WAGENI – MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Seriali ipo makini na ajira za wageni na itaendelea kuhakikisha kuwa Watanzania wanapewa fursa kwanza.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Leah Komanya aliyetaka kupata kauli ya Serikali juu ya wageni wanaoingia nchini na kupata ajira kwenye maeneo nyeti kama vile bandarini au viwanja vya ndege.

“Ajira zote za wageni nchini Tanzania ni kwa nafasi zile za kitaalam tu ambazo Watanzania hawana uwezo nazo na hatujaacha wazi, tumeweka ukomo kuwa ni wageni watano tu kwa kila taasisi ndio wanapata fursa ya kuajiriwa ndani ya nchi, kuitumikia taasisi hiyo na ni kwa nafasi ambazo watanzania hawana uwezo nazo,” amesisitiza. 

Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu amesema pale ambapo italazimu raia wa nje apate ajira, Serikali itaendelea kusimamia ili kuhakikisha kama kweli nafasi hiyo haina mtu na ni nafasi nyeti yenye utaalam ambao hakuna Mtanzania mwenye uwezo nayo.

Akijibu hoja kuhusu wageni kufanya kazi kwenye maeneo nyeti, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba hakuna mgeni anayefanya kazi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege, bandari au yale ya mipakani. “Hii ni kwa sababu ni lazima tuweke Watanzania ambao kweli wanakerwa na nchi yao na wanaweza kulinda nchi yao kuanzia mipakani ili kuhakikisha kwamba hakuna jambo lolote linaloashiria kuvunjika kwa amani.”

Amesema endapo atakutwa mtu yeyote wa Taifa la nje anafanya kazi kwenye maeneo hayo, basi atakuwa ameajiriwa na kampuni ambayo inafanya shughuli maalum kwenye eneo hilo na kwa masharti yale yale kwamba watapata nafasi kufanya kazi kwenye kampuni hiyo kama nafasi hiyo hakuna Mtanzania mwenye uwezo nayo.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, MEI 17, 2018.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com