Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, akipeana mkono na Makamu Mkuu wa Shirika la Don Bosco Kanda ya
Afrika, Augustine Sellam katika viwanja vya Don Bosco, kwenye uzinduzi wa
mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana na uwekaji wa kumbukumbu ya miaka 100 ya
ILO, jijini Dodoma, Septemba 14.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia vipuri
vilivyo chongwa na wanafunzi wa Chuo cha Don Bosco Dodoma, kwenye uzinduzi wa
mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana na uwekaji wa kumbukumbu ya miaka 100 wa
ILO, uliyofanyika katika viwanja vya Don Bosco, jijini Dodoma, Septemba
14.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia mfano
wa nyumba uliyojengwa na matofali ya kisasa ya kupachika , kwenye uzinduzi wa
mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana na uwekaji wa kumbukumbu ya miaka 100 wa
ILO, uliyofanyika katika viwanja vya Don Bosco, jijini Dodoma, Septemba
14.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema zaidi ya vijana 46,000 wanatarajiwa kunufaika
na mafunzo ya stadi za kazi kwa njia ya
uanagenzi kupitia taasisi ya Don
Bosco Net Tanzaniakatika mwaka huu wa fedha.
Ameyasema hayo
leo (Jumamosi, Septemba 14, 2019) wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo na maadhimisho
ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO), katika viwanja
vya Donbosco jijini Dodoma.
“Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imeandaa Programu ya
Kukuza Ujuzi Nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi
kwa vijana wa ngazi mbalimbali za elimu kuanzia wahitimu wa darasa la saba hadi
vyuo vikuu.”
Waziri
Mkuu amesema miongoni mwa mafunzo yanayotolewa chini ya programu hiyo ni ya
uanagenzi (apprenticeship) ambayo yalianza 2017 na 2018 walihitimu vijana
32,786.
Waziri
Mkuu amesema katika awamu ya pili ya mafunzo hayo yaliyozinduliwa leo ambayo
yanahusisha jumla ya vijana 5,875kama
sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 ya ILO.
Amesema
licha ya mafanikio yaliyoonekana katika sekta ya Kazi na Ajira kwa kipindi cha
miaka 100 iliyopita, suala la ukosefu wa ajira kwa vijana ni miongoni mwa
changamoto inayoikabili dunia, hivyo linahitaji kuwekewa mikakati endelevu kwa
miaka 100 ijayo.
Waziri Mkuu
amesema miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia ukosefu wa
ajira kwa vijana ni vijana kutokuwa na ujuzi sahihi wa kuwawezesha kujiajiri au
kuajiriwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema hadi kufikia Juni 2019 jumla ya
vijana 36,726 wamefaidika na programu ya kukuza ujuzi inayogharamiwa na
Serikali wa asilimia 100.
Amesema
kati yao vijana 6,455 walinufaika na mafunzo ya uanagenzi katika fani
mbalimbali zikiwemo za ushonaji na nguo, useremara, uashi, terazo, uchongaji wa
vipuri, ufundi magari, umeme na utengenezaji wa viatu vya ngozi.
Waziri
huyo amesema mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa
mafunzo yametolewa kwa vijana 10,443 katika fani za uashi, useremara, ufundi wa
magari, upishi na huduma za hoteli.
Pia,
Waziri Jenista amesema kwa upande wa mafunzo ya kilimo cha kisasa jumla ya
vijana 18,800 walinufaika na mafunzo hayo huku vijana wengine 1,028 walipatiwa
mafunzo ya vitendo pahala pa kazi.
Naye,
Mratibu wa Miradi wa Taasisi ya Donbosco Tanzania, Rosemary Terry Njoki amesema
programu ya kukuza ujuzi imezingatia kuwawezesha vijana wa miaka kati 17 hadi
35 kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Amesema
mafunzo hayo yataliwezesha Taifa kufikia lengo lake ya kukuza uchumi kutoka wa
chini kwenda wa kati ifikapo 2025 kwa kuwa yatakuwa yameongeza wafanyakazi
wenye ujuzi ambao wanahitajika kwa wingi.
Awali, Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki,
Wellington Chibebe amesema shirika hilo limedhamiria kupigania haki ya kijamii
pamoja na haki za binadamu na kazi zinazotambulika kimataifa.
Amesema tangu
mwaka 1919, ILO ni shirika pekee la Umoja wa Mataifa lenye mfumo wa utatu
unaowaleta pamoja wafanyakazi, waajiri na Serikali katika nchi 187 wanachama wa
shirika hilo katika kuweka viwango vya masuala ya kazi, kukuza sera na kupanga
programu za zinazochagiza kazi zenye staha kwa watu wa jinsia zote.
“Maadhimisho
ya karne moja ya ILO ni fursa nzuri ya kujitathimini wapi lilipotoka,
kusheherekea historia na mafanikio yake na pia kutafakari siku zijazo. Pia ni
jukwaa la kipekee la kuihakikishia dunia umuhimu wa jukumu na mamlaka yake
ya kutetea haki ya kijamii na ajenda ya kazi zenye staha”
Baada ya uzinduzi
huo, Waziri Mkuu alishiriki shughuli ya kupanda jumla ya miti 200 katika Mji wa
Serikali, Mtumba kuashiria miaka 100 ya ILO iliyopita na miaka 100 ijayo.
0 comments:
Post a Comment