Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka
akizungumza na walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika Hafla fupi ya
kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, aliyofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, aliyofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kwa kuongeza ufaulu, aliyofanyika Mjini Bariadi.
Na
Stella Kalinga, Simiyu
Mkoa wa Simiyu umejipanga kuanza kuwaandaa
Wanafunzi wa Darasa la Saba na Kidato cha Nne wa mwaka 2019 kuanzia mwezi
Agosti, mwaka huu 2018 ili kufikia malengo ya kuongeza ufaulu katika mitihani
yote ya Taifa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa
huo Mhe. Anthony Mtaka katika Hafla fupi ya kuwapongeza walimu wa Halmashauri
ya Mji wa Bariadi kwa kuongeza ufaulu kwa Shule za Msingi na Sekondari kipindi
cha miaka miwili mfululizo, iliyofanyika Ukumbi wa Bariadi Alliance Mjini hapa.
Mtaka amesema kutakuwa na mitihani
kwa wanafunzi wa darasa la sita na kidato cha tatu mwezi Agosti 2018 ili
kupata wanafunzi wenye ufaulu mzuri watakaounda darasa maalumu la darasa la
saba na kidato cha nne mwaka 2019 ( special class).
"Tunaanza maandalizi ya darasa
la saba na kidato cha nne wa mwakani kuanzia mwezi Agosti mwaka huu, ili
tuchuje bila kupendelea mtihani ni chujio zuri, matokeo hayo yatabandikwa na
wazazi wote wataona" alisema Mtaka.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema
baada ya kumaliza kambi ya kitaaluma kwa kidato cha sita mwezi huu, Mkoa
umepanga kufanya kambi za kitaaluma kwa kidato cha nne na darasa la saba ambazo
zitafunguliwa rasmi tarehe 06 Juni, 2018.
Wakati huo huo amesema Serikali
inaendelea kuwajengea uwezo walimu mahiri na makini ili waweze kuwasaidia
wanafunzi wa madarasa maalumu kufanya vizuri lengo likiwa ni kuongeza ufaulu
kwa shule za msingi na kufuta daraja la nne na sifuri kwa shule za sekondari.
Kuhusu ujenzi wa Shule ya Sekondari
ya Mkoa, Mtaka amesema Mkoa utajenga shule ya Mkoa Mjini Bariadi (Makao Makuu
ya mkoa) ambayo itatambulika kama Shule ya Sekondari Simiyu na itakuwa na uwezo
wa kuchukua wanafunzi 1000 huku ikiwa na miundombinu mingine muhimu kama
maabara, vyumba vya kompyuta na mkongo wa Taifa.
Pia amesema pamoja na kujenga Shule hiyo
ya Mkoa, Serikali imedhamiria kwa kushirikiana na wananchi kujenga shule mbili
maalumu kwa ajili ya wasichana na wavulana (Simiyu Girls na Simiyu Boy's)
ambazo zitabeba taswira ya Mkoa na kutambulisha Mkoa huo tofauti na ilivyo sasa
ambapo shule nyingi zilizopo katika Makao makuu ya Mkoa ni zile za Kata.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa
Mkoa amewaruhusu walimu mkoani humo kufundisha masomo ya ziada (tuition)
hususani wakati wa likizo na mapumziko ili wanafunzi waendelee kujifunza badala
ya kusubiri kufundishwa darasani pekee.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wa
Halmashauri ya Mji, Mwl. Travel Ndimangwa kutoka Shule ya Msingi Somanda A
amepongeza utaratibu wa kuwaandaa wanafunzi wa madarasa ya mitihani pamoja na
kuruhusiwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya ziada mambo ambayo amesema
yatachangia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi, Mhe. Robert Lweyo ametoa wito kwa walimu wa Halmashauri hiyo kufanya
kazi kwa bidii na weledi ili kupandisha ufaulu ambapo mwaka 2017 ilishika
nafasi ya 22 Kitaifa katika mtihani wa Kidato cha Nne kutoka nafasi ya 44 mwaka
2016.
0 comments:
Post a Comment