METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, January 22, 2019

“MAMBO YA 7 YA MFANO, MIEZI MIWILI BAADA YA MIAKA MITATU YA RAIS MAGUFULI”


Na Debora Charles Kiyuga✍🏽

Ni dhahiri kuwa mafanikio ya Uongozi Bora wa Mhe. Rais Daktari John Pombe Joseph Magufuli yamekuwa yakitambulika ndani na nje ya nchi na hata kupelekea kiongozi huyu kutunukiwa TUZO mbalimbali za heshima kimataifa. 

Mfano hivi karibuni tumeshuhudia Jarida la Mtandaoni la Afrika 54 likimbainisha kiongozi huyu kushika nafasi ya pili kati ya marais watano Bora barani Afrika kwa mwaka 2018 kutokana na kazi aliyoifanya ndani ya miaka mitatu ya utawala wake, hasa katika kuwezesha elimu bure, kufufua Shirika la ndege na kununua ndege 7, kujenga Reli Mpya ya Kisasa (SGR), kuongeza upatikanaji wa huduma za afya pamoja na kupiga vita rushwa na ufisadi. 

Kipindi hiki pia, tumeshuhudia akitangazwa kuwa mshindi wa TUZO ya Uongozi katika Siasa kwa mwaka 2018 iliyotolewa na Jarida Mashuhuri la African Leadership Magazine (ALM) lililoko Uingereza, ushindi ambao umetokana na mafanikio ambayo Tanzania imepata chini ya uongozi wake.

Tukiwa tunaelekea mwezi wa tatu baada ya miaka mitatu ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tangu kuapishwa kwake tarehe 05 Novemba, 2015 kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Awamu ya Tano, Ni dhahiri kuwa Tanzania inaendelea kuwa IMARA na ya Maendeleo. 

Tumeshuhudia kuwa uchumi wa Taifa letu bado unaendelea kuwa imara, ukikua kwa asilimia 7.1 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa asilimia 7.0 kwa miaka miwili iliyopita (2015-2016) ambapo hivi karibuni, Taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango kwa vyombo vya Habari kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa na Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali iliyotolewa tarehe 30 Disemba, 2018 jijini Dar Es Salaam ilibainisha huku ikionyesha kuwa Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi 5 bora kwa kasi ya ukuaji wa uchumi katika bara la Afrika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2018. 

Kadhalika Pato la Taifa limeendelea kukua kwa asilimia 7.0 kwa kipindi cha Januari hadi June 2018 ikilinganishwa na asilimia 6.3 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2017. Yafuatayo ni mambo saba ya mfano katika kipindi cha miezi miwili baada ya miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Magufuli; 

Mosi, Utolewaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Tarehe 10 Desemba, mwaka jana katika Mkutano wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwa ajili ya majadiliano yanayohusu mapato ya fedha ya nchi,  Rais John Pombe Magufuli alizindua vitambulisho 670,000 ambavyo vilikabidhiwa kwa Wakuu wa Mikoa kwa ajili ya matumizi ya wajasiriamali wadogo wadogo wenye mitaji ya thamani chini ya Milioni 4 katika mikoa yote ya Tanzania Bara. 

Kila mkoa vilitolewa vitambulisho elfu 25 ambapo tayari mikoa mingi imekwisha tekeleza agizo hilo. Utolewaji wa vitambulisho hivi ni muendelezo wa Serikali kuhakikisha inatetea haki za wanyonge kutokana na lengo kuwa kila anayepata kitambulisho hiki hapaswi kusumbuliwa kulipa kodi.

Pili, kuanza kwa upanuzi wa barabara yenye urefu wa Km 19.2 kutoka Kimara hadi Kibaha kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 141.5 zinazotokana na kodi za watanzania ambayo ikikamilika itakuwa na njia 8, barabara ambayo ilizinduliwa hivi karibuni tarehe 19 Disemba, 2018 na Mhe Rais Magufuli. Ikumbukwe kuwa, Ubungo ni sehemu ya jiji la Dar es salaam, jiji la biashara ambalo ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi kubwa katika Afrika. 

Tafiti zinaonyesha kuwa itakapofika mwaka 2030 Dar es Salaam itakuwa miongoni mwa majiji matano makubwa (Major Cities) kwa idadi ya watu Barani Afrika ikiungana na majiji mengine kama Cairo, Lagos na Rwanda ambayo yatakuwa na idadi ya zaidi ya watu milioni 10. Ili kuendana na ongezeko hilo kubwa la watu, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu pamoja na kuboresha huduma za jamii katika jiji hili, ikiwemo upanuzi wa barabara hii kutoka njia 2  hadi 8.

Tatu, Uwekaji wa jiwe la msingi wa Daraja la Salender. Tarehe 23 Julai, 2018 tulishudhudia Waziri Mkuu wa Korea akishiriki zoezi la uwekaji saini wa mkataba wa ujenzi wa daraja la Salender ambapo miezi mitano baadae Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya nchi hiyo iliweka jiwe la msingi la mradi huu. Mradi huu utahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa Kilometa 1.03 ambalo litakuwa refu zaidi hapa nchini kwa sasa likifuatiwa na daraja la Rufiji lenye mita 970.5, Daraja la mto Ruvuma lenye mita 720,  Daraja la Nyerere Kigamboni lenye mita 680 na Daraja la Magufuli Kilombero lenye mita 384. 

Mradi huu utaboresha mandhari ya jiji la Dar es Salaam, utataua kero ya foleni na utapunguza upotevu wa mapato ya nchi kwa takribani shilingi bilioni 400 kwa mwaka kwa saababu ya foleni. Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya kiasi cha shilingi bilioni 556.1. Ushirikiano baina ya kutekeleza mradi huu kwa Serikali hizi mbili za Tanzania na Korea Kusini ni muendelezo wa mahusiano mazuri na utekelezaji wa miradi mingine kama vile ujenzi wa hospitali ya Mloganzila pamoja na Daraja la Kikwete kwenye mto Maragarasi.

Nne, Upokeaji wa ndege mpya 2 aina ya Airbus A220- 300. Hivi karibuni tumeshuhudia nchi yetu ya Tanzania ikivunja rekodi ya kupokea ndege mbili za aina ya Airbus A220-300 zilizonunuliwa na Serikali ya Tanzania ikiwa ni ndege za kwanza za aina hii kuingia Afrika. Ujio wa ndege hizi 2 ulikuwa umekamilisha idadi ya ndege 6 ambazo tayari zimekwisha ingia nchini. 

Mwishoni mwa mwaka huu tunategemea kupokea ndege nyingine ya 7 aina ya Dreamliner kutoka Marekani yenye uwezo wa kubeba watu 262 na hivyo kuzifanya ziwe 2 nchini, ndege ambazo zitakuwa zinapishana katika masafa ya ndani na nje ya Afrika. Pia Serikali imenunua ndege nyingine aina ya Bombardier na hivyo kukamilisha idadi ya ndege 8 na inaendelea kukarabati ndege nyingine ya Bombardier Q300 iliyokuwepo tangu mwanzo na hivyo kukamilisha idadi ya ndege 9. Pamoja na hayo, Rais Magufuli alitoa ndege za Rais 2 na kuagiza zipakwe rangi ya Air Tanzania ili ziwe zinabeba abiria kwa siku ambazo hazitumiwi na Rais.

Tano, Usimikaji wa nguzo za umeme katika Reli Mpya ya Kisasa (Standard Gauge Railway). Kazi ya Usimikaji wa Nguzo za Umeme utakaotumika Kuendesha treni za Kisasa zitakazotumia Umeme na Reli ya kisasa - SGR ilianza mapema Disemba, 2018 katika eneo la Soga nje Kidogo ya Kambi ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa iliyopo Soga mkoani Pwani. Nguzo hizo zinajengwa umbali wa Mita 50 kutoka nguzo moja hadi nyingine, urefu wa nguzo moja ni Mita 9.5 huku uzito wa nguzo Moja ukiwa wa Tani 2.4. Nguzo hizi zina uwezo wa kudumu kwa kipindi cha Miaka 120 pia zimewekewa madini ya Zinki kwa ajili ya kuzuia kutu. 

Ujenzi wa Reli hii unakadiriwa kuongeza maradufu biashara ya nchi na mataifa mengine, kuimarisha na kukuza sekta nyingine nchini, kuwezesha malighafi kusafirishwa kwenye maeneo ya viwanda, kuwezesha bidhaa zinazozalishwa viwandani kusafirishwa kwenye masoko husika kwa wakati na kwa haraka, kukuza sekta ya utalii, kusaidia kutunza barabara na kuongeza ajira kwa watanzania wengi.  

Sita, Kusitishwa kwa matumizi ya Kikokotoo Kipya. Kufuatia kutambua heshima ya kustaafu kwa wafanyakazi hivi karibuni Rais Magufuli aliagiza kikokotoo kilichokuwa kinatumika kwa kila mfuko kabla ya mifuko kuunganishwa kiendelee kwa kipindi cha mpito hadi mwaka 2023. Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 20 Octoba, 2017 Serikali kupitia Baraza lake la Mawaziri ilipitisha uamuzi wa kuunganisha mifuko ya pensheni ambayo ilikuwa ni Mfuko wa pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa PPF, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali (GEPF) na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), ili  kuunda mfuko mmoja wa Pensheni kwa ajili ya Watumishi wa Umma. 

Kadhalika ilikubaliana Mfuko wa NSSF ufanyiwe marekebisho ili uwe kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta binafsi pamoja na sekta isiyo rasmi, hatua ambayo ilitokana na ombi la muda mrefu la Vyama Vya Wafanyakazi kutaka mifuko iunganishwe kwa sababu ilisadikika mifuko hii ilikuwa inakwenda kufa na mnamo tarehe 31 Januari, 2018, Bunge lilipitisha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma. 

Saba, Serikali kukabidhiwa Mfumo wa Usimamizi wa Simu. Sekta ya mawasiliano hasa mawasiliano ya simu ni sekta nyeti na muhimu ambayo hivi sasa inakuwa kwa kasi kubwa duniani, takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu bilioni 5 wanatumia simu za mkononi duniani kote na na watu bilioni 3.9 wanatumia huduma za vifurushi yaani data. Mpaka sasa katika nchi yetu ya Tanzania, idadi ya watu wenye simu za mkononi imefikia milioni 42,961 na wenye kutumia vifurushi yaani bando wamefikia milioni 22,995. Idadi  hii kubwa ya watumiaji wa simu za mkononi na vifurushi imeongeza kasi ya upashanaji wa habari duniani na kupelekea kukua kwa sekta ya mawasiliano. 

Sekta ya mawasiliano imechochea shughuli za kiuchumi na kijamii duniani, ikiwemo kuongeza uzalishaji viwandani, kupatikana kwa huduma mbalimbali ambazo aghalabu zamani hazikuwepo mfano huduma za elimu na afya kwa njia ya mtandao (E- Education na E- Health), huduma za usafiri kwa tax kama vile uber na Taxify, huduma za kibenki ambapo hapa nchini kwetu watu waliojisajiri na huduma za kifedha kwenye simu wanafikia mil 20.85 na hii ndiyo iliyochangia nchi yetu kuibuka kinara wa uchumi Jumuishi kwa nchi zilizopo kusini mwa Bara za Afrika. 

Licha ya manufaa haya, sekta hii imesababisha changamoto ikiwepo uharibifu wa matumizi ya kimtandao na kuongezeka kwa mmonyoko wa maadili katika jamii. Ili kukabiliana na changamoto hizi Serikali ya Tanzania imeanzisha Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa TCRA, ambapo imetunga sera, sheria, kanuni na kujenga miundombinu mbalimbali ya mifumo ya Udhibiti na Usimamizi ikiwemo mfumo wa TTMS ambao ulikabidhiwa Serikalini hivi karibuni ikiwa kazi yake kubwa ni kufuatilia mawasiliano ya simu za ndani, kimataifa zinazofanyika nchini, kwa njia ya sauti, matumizi ya data na jumbe fupi.

ITAENDELEA.

Debora Charles Kiyuga
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Share:

1 comment:

  1. Umechambua vizuri sana.

    Mungu ambariki Rais wetu ili aendelee kurejesha heshima ya Tanzania ndani na nje ya Afrika

    ReplyDelete

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com