METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, March 26, 2018

WAFANYABIASHARA TUMIENI TAASISI ZA KIFEDHA KUKUZA MITAJI YENU-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wilayani Ruangwa kutumia taasisi za kifedha kukopa fedha kwa ajili ya kukuza mitaji yao.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Machi 25, 2018) wakati akizungumza na wafanyabiashara wa wilaya hiyo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Walimu, wilayani Ruangwa.

Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amesema ni vema wakatumia taasisi za kifedha zilizopo ili kukuza mitaji yao.

”Naamini sekta ya biashara ni muhimu katika mabadiliko ya maendeleo, hivyo wafanyabiashara ni chachu ya maendeleo kokote na Serikali itaendelea kuwaunga mkono.”

Amesema katika kuhakikisha riba zinapungua, Rais Dkt. John Magufuli anaendelea kuzungumza na wamiliki wa taasisi za kifedha ili waone namna ya kupunguza riba hiyo.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali la kuchukua hatua hiyo ni katika kutekeleza mkakati wake wa  kuwawezesha wafanyabiashara ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu.

Pia Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba Serikali ipo pamoja nao na imedhamilia kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama maji na afya.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Said Shea amewaomba wafanyabiashara wenzake watumie fursa za maendeleo zilizoko wilayani humo kwa kupanua wigo wa biashara zao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 25, 2018.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com