METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 16, 2018

Ujenzi wa barabara Buswelu-Sabasaba Manispaa ya Ilemela kuanza rasmi

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela John Wanga akizungumza katika kikao cha  Baraza la Madiwani jana kilichofanyika katika ukumbi  halmashauri hiyo.
Judith Ferdinand-BMG Habari
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya kwa kiwango cha lami kutoka Buswelu hadi Sabasaba kuanzia mwezi Mei mwaka huu.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 9.7 ni kiunganishi kikuu cha maeneo ya Buswelu, Kiseke hadi Sabasaba ambapo hata hivyo awali mradi huo ulielezwa kuanza huu.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga aliyasema hayo jana kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo na kuongeza kwamba huo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya uchaguzi mkuu 2015 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo halmashauri hiyo iliridhia kutekeleza mradi huo.
“Nipende kulijulisha baraza hili kuwa kazi ya ujenzi itaanza mwezi Mei mwaka huu badala ya mwezi Machi kama taarifa ilivyotolewa katika baraza lililopita kwani mpaka sasa taratibu za zabuni zimakamilika”. Alisema Wanga.
Wanga alisema barabara hiyo imefadhiliwa na serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia kupitia mradi wa Uendelezaji Miji na Majiji (TSCP) kwa kushirikiana na halmashauri hiyo.
Pia alisema hadi sasa kiasi cha shilingi 306,008,000  zimelipwa fidia kwa wananchi 22 kati ya shilingi 636,626,000 zilizotengwa, hivyo zoezi la uhakiki na ulipaji fidia bado linaendelea na waliolipwa baadhi wamevunja nyumba zao ikiwa ni pamoja na kukata miti ili kuacha wazi eneo la mradi.
Hata hivyo alitoa wito kwa madiwani na wananchi kwa ujumla kushirikiana wakati wa utekelezaji wa mradi huo pindi utakapoanza kutekelezwa ili kusiwe na mkwamo utakaotokana na malalamiko yasiyokuwa ya msingi.
Aidha alisema ili kuleta  taswira nzuri ya halmashauri, wanatekeleza miradi hasa ya kujenga barabara ikiwemo hiyo ya Buswelu, barabara ya Mji Mwema-Bigbite na Mwaloni-Kigoto kwa kiwango cha lami.
Naye Meya wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga alisema halmashauri hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kupitia kamati mbalimbali na kuwataka viongozi kuendelea kuwa na ushirikiano wa kutosha katika kuleta maendeleo.
Meya wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulinga akizungumza katika kikao cha baraza la badiwani kilichofanyika jana katika ukumbi halmashauri hiyo.
Diwani wa Kata ya Shibula, Dede Swila akichangia mada katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Diwani wa Kata ya Nyasaka, Shabani Maganga akichangia mada katika kikao hicho.
Diwani wa Kata ya Buswelu, Sarah Ng’wani akichangia mada katika kikao cha Baraza la madiwani halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kilichoketi jana kwenye ukumbi halmashauri hiyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com