METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 26, 2018

WAKULIMA WADOGO WA CHAI WAPEWE KIPAUMBELE KWANZA: DKT MWANJELWA


Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati alipotembelea Kituo cha kupimia chai ya Wakulima wadogo wa Kijiji cha Luangu Kata ya Kifanya na Tarafa ya Igominyi katika Wilaya ya Njombe
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akiangalia naomna zoezi la upimaji wa chai ya Wakulima wadogo kama lilivyokuwa likiendeshwa na Wawakilishi wa Kampuni ya NOSC katika mashamba ya Wakulima wadogo wa Kijiji cha Luangu Kata ya Kifanya na Tarafa ya Igominyi katika Wilaya ya Njombe
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akiwa na Mbunge wa Njombe Mwalongo Edward pembeni yao ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Njombe Mji Bwana Edwin Mwenzili na Diwani wa Kata ya Kifanya Nolasco Mtewele
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akiwa na Mbunge wa Njombe Mwalongo Edward wakiangalia mche bora wa parachichi aina ya Hass katika kitalu cha shama la Taasisi ya TAHA katika Halmashauri ya Mji wa Njombe


Na Mwandishi Maalumu

Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa amewaagiza Kampuni ya NOSC kuendelea kununua kiasi kikubwa cha Chai ya Wakuliwa wadogo kwanza kabla ya kufikiria kununua kwa Wakulima wakubwa.

Dkt. Mwanjelwa amesema amefurahishwa na utendaji wa Kampuni ya NOSC baada ya kujirisha kuwa Kampuni hiyo imekuwa ikinunua zaidi ya asilimia 80 ya chai ya Wakulima wadogo.

Kampuni ya NOSC ni Kampuni iliyojikita katika kununua cha ya Wakulima wadogo na wakati huo huo wanauza chai hiyo kwa Kampuni ya usindikaji wa chai ya Uniliver

Aidha, Dkt Mary Mwanjelwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano kwa nia njema imeamua kuboresha uzalishaji wa mazao ya kimkakati Chai likiwa zao moja wapo na kwamba maisha ya Wakulima wanaolima chai yatakuwa bora kama Wakulima hao wataendelea kuwa na uhakika wa soko na la bei nzuri.

Naibu Waziri aliyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara mbele ya Wakulima wa chai wa Kijiji cha Luangu Kata ya Kifanya na Tarafa ya Igominyi katika Wilaya ya Njombe na kuwahamasisha kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangamkia fursa ya kulima zao la chai ili kuongeza tija na uzalishaji kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa Serikali imeamua kutilia mkazo kwenye kuongeza tija na uzalishaji kwenye mazao matano ya kimkakati lengo ni kuwasaidia Wakulima kuinua maisha yao na wakati huohuo kuliongezea taifa akiba ya fedha za kigeni.

Naibu Waziri ameyataja mazao ya kimkakati kwa ni pamoja na pamba, kahawa, chai, tumbaku na katani.

Katika mkutano huo, Dkt. Mwanjelwa amewahamasisha Wakulima hao kuongeza eneo la kilimo cha chai kwa kuwa tayari Serikali imeanza kuboresha miundombinu ya barabara kutoka mashambani mpaka katika kiwanda cha Uniliver na kuongeza kuwa Taasisi ya Kizalendo ya NOSC imekuwa mkombozi wa kweli kwa kununua chai yao kwa bei nzuri ya shilingi 307.11.

Mbali na Taasisi ya NOSC kununua chai ya Wakulima kwa bei na baadae kuiuza katika Kiwanda cha Uniliver Taasisi hiyo pia imekuwa ikiwakopesha Wakulima hao pembejeo za kilimo bila riba kuanzia hatua ya kwanza mpaka ya mwisho na kisha kuwakata baadae wanapoaza kuvuna chai yao katika kipindi cha miaka mitatu.

Naibu Waziri amewaasa Wakulima kufuata masharti na elimu ya kilimo cha chai kwa kuwa bila ya kufanya huvyo wasitarajie matokeo bora.

“Pandeni na mfuate masharti ya Wataalam ili mpate matokeo bora na kwa kufanya hivyo nasisitiza, kipaumbele apewe Mkulima mdogo na anayefanya vizuri”. Amekaririwa Dkt Mwanjelwa.

Naibu Waziri ameipongeza Kampuni ya NOSC kwa kuwapa kipaumbele Wakulima wazawa ambapo kiasi cha zaidi ya asilimia 80 ya chai ya Wakulima hao imekuwa ikinunuliwa na kwa bei ya juu ukilinganisha na maeneo mengine yanayolima chai nchini.

NOSCI ni kifupi cha maneno Njombe Out – growers Service Company. Ni Kampuni ya Kizalendo ambayo lengo lake ni kutoa msaada wa kitaalam kwa Wakulima wadogo wa Mkoa wa Njombe kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi kwenye kilimo cha chai na wakati huohuo kuhakikisha kuwa zao la chai linapandwa na kuendelezwa kwa kufuata utaalam na kwa kumsaidia Mkulima kupata mazingira wezeshi ya kuendesha kilimo cha chai.

Kampuni ya NOSC inafanya kazi bega kwa bega na Kampuni ya Uniliver lengo likiwa ni kuhakikisha walau hekta 3,800 zinapatikana na kuendelezwa na Wakulima wadogo wa chai Mkoani Njombe.

Dkt. Mwanjelwa amesema ni vyema Wakulima wa Njombe wakatumia mapato yanayotokana na kilimo cha chai kuboresha maisha yao.

“Tumieni mapato mnayopata kwenye chai kuboresha maisha yenu na kwa kufanya hivyo, mtaiweka Njombe kwenye ramani ya Dunia” Amekaririwa Naibu Waziri.

Wakati huohuo Naibu Waziri ametumia nafasi hiyo kukitembelea Kituo cha kuhifadhi matunda na kuyafunga tayari kwa kupeleka nje ya nchi. Kituo kilichojengwa kwa fedha za Serikali kwa ajili ya kuwasaidia Wakulima wa matunda aina ya parachichi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Dkt. Mwanjelwa amesifu juhudi zinazofanya na Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa kuratibu na kujenga mazingira mazuri ya kuwaunganisha Wakulima wa matunda hayo na masoko ya kimataifa yaliyopo Ulaya na Amerika.

Walipokuwa Kituoni hapo Mbunge wa Jimbo la Njombe Mhe. Edward Mwalongo amewasilisha ombi kwa Naibu Waziri kuhusu Wakulima wa Jimbo lake kupatiwa miche bora ya zao la parachichi kama ilivyo kwenye miche ya zao la korosho.

Akijibu ombi hilo Naibu Waziri amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kutenga fedha za kutosha kwenye Bajeti yao kwa ajili ya kugharamia shughuli za kilimo na kusisitiza kuwa Halmashauri zinapaswa kutenga walau asilimia ishirini ya bajeti zao kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa kuwa kilimo kinagusa maisha ya Wananchi wengi.

MWISHO
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com