Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary
Mwanjelwa akihutubia sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Luguya Kata ya Mtwango na
Tarafa ya Makambako wakati wa Mkutano wa hadhara
Mbunge wa Jimbo la Lupembe Mhe. Joram
Hongoli kumueleza Naibu Waziri wa Kilimo kero mbalimbali za Wakulima wa Jimbo
hilo katika mkutano huo mapema leo
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary
Mwanjelwa akipokea risala kutoka kwa Mwanakikundi cha Wakulima wa viazi
mviringo wa Kijiji cha Luguya
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary
Mwanjelwa akiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Lupembe Mhe. Joram Hongoli wakiwa
katika shamba la Mkulima wa mbegu za viazi mviringo Bibi Sara Nyagawa katika
Kijiji cha Maduma Kata ya Kichiwa katika Wilaya ya Njombe
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary
Mwanjelwa akiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Lupembe Mhe. Joram Hongoli
sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Ruth Msafiri pamoja na Mkulima wa
mbegu za viazi mviringo Bibi Sara Nyagawa katika Kijiji cha Maduma Kata ya
Kichiwa wakitoka shambani na kusindikizwa na ngoma ya Wanakijiji katika ziara
hiyo
1 Sehemu ya umati wa Wananchi wa Jimbo la
Lupembe wakimuaga Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa mara baada
ya kuhitimisha ziara yake katika jimbo hilo.
Naibu Waziri wa Wizara
ya Kilimo Dkt Mary Mwanjelwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitasita
kumchukulia hatua kali Wakala yeyote atakayebainika kuvunja sheria na taratibu
za nchi.
Dkt Mwanjelwa alitoa
onyo hilo wakati wa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kijiji cha Luguya Kata
ya Mtwango na Tarafa ya Makambako mara baada ya Mbunge wa Jimbo la Lupembe Mhe.
Joram Hongoli kumueleza kuwa Wakulima wa Jimbo hilo wamekuwa wakihangaika kupata
pembejeo za kilimo, zikiwemo mbolea za kupandia na kukuzia.
Mbunge huyo amemueleza Naibu
Waziri huyo wa Kilimo kuwa kumekuwa na juhudi za makusudi za kuwahujumu
Wakulima ambapo mbolea imekuwa ikifika katika Mkoa wa Njombe kutoka bandarini
Dar es Salaam na baada ya muda mfupi ukosekana sokoni na chache inayopatikana
uuzwa bei ya juu tofauti na bei elekezi ya Serikali.
“Mhe. Naibu Waziri hiki
ni kilio cha Wananchi wa Jimbo letu la Lupembe na kama unavyofaham kilimo ndiyo
shughuli yetu ya msingi katika maisha ya kila siku, kukosekana kwa mbolea
kunarudisha nyuma juhudi za Wananchi wengi” Amekaririwa Mbunge Hongoli.
Dkt Mwanjelwa amesema
kilimo ni Sekta wezeshi ya kusukuma mbele juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya
kufikia uchumi wa viwanda ambapo bila malighafi zinazotokana na mazao ya
kilimo, kamwe Serikali haiwezi kukaa kimya na kufumbia macho hujuma za
Mawakala.
“Nataka Mawakala wote
wanaouza mbolea kote nchini, wafahamu kuwa ni marufuku kuficha mbolea au kuuza kinyume
cha bei elekezi, ole wake kwa atakayeshindwa kuenenda sawa na matakwa ya
Serikali”. Ameonya Dkt. Mwanjelwa.
Dkt. Mwanjelwa amesema
kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga ili kuhakikisha kuwa msimu wa kilimo unaokuja,
mbolea itapatikana mapema na itafika katika Mikoa yote kwa wakati.
Akiongelea kuhusu soko
la mazao ya jamii ya nafaka kama mahindi, Dkt Mwanjelwa, amesema Serikali
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao
Mchanganyiko zote kwa pamoja zitapewa fedha za kutosha ili kununua mazao ya
Wakulima kwa wingi.
“Tumedhamiria
kuimarisha Taasisi yetu ya NFRA na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na kwa
kuwa Bodi ya Nafaka imepewa Mamlaka ya Kisheria ya kufanya biashara,
nawahakikishia kuwa Bodi itanunua mazao ya Wakulima na kuongeza kuwa bado
Wananchi wana nafasi ya kufanya biashara ya mazao ya kilimo kwani Serikali
imefungua mipaka kwa kila mwenye nia na uwezo wa kuuza mazao nje ya nchi
kuufanya”. Amekaririwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Wakati huohuo Dkt
Mwanjelwa alipata nafasi ya kumtembelea Mama Sara Nyagawa mkulima mzalishaji wa
mbegu za viazi mviringo wa Kijiji cha Maduma Kata ya Kichiwa katika Wilaya ya
Njombe.
Naibu Waziri
alimpongeza Mama Sara Nyagawa kwa kuwa mkulima bora wa kuzalisha mbegu bora za
viazi na kuongeza kuwa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini
yaani SAGCOT imekuwa chachu ya mafanikio hayo.
Dkt Mwanjelwa amesema
Sara Nyagawa amekuwa mfano wa kuigwa na kuongeza kuwa Wakulima ambao wanalima
viazi mviringo kama wanataka kupata mazao bora ni vyema kama watajikita katika
kutumia mbego bora kwa kuwa tija na uzalishaji mkubwa unaanzia kwenye mbegu.
“Natoa wito, ili
Wakulima wa viazi mviringo wapate masoko ya mazao yao ni vizuri wakaanza kwanza
kulima kwa kutumia mbegu bora”. Amekaririwa Naibu Waziri.
0 comments:
Post a Comment