Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akiangalia alama ya kimataifa
katika mpaka baina ya Tanzania na Kenya eneo la Serengeti Wilaya ya Tarime mkoa
wa mara wakati wa ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akiangalia eneo la mpaka baina ya
Tanzania na Kenya katika eneo la
Serengeti Wilaya ya Tarime mkoa wa mara wakati wa ziara yake ya kukagua mpaka
wa Tanzania na Kenya.
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya makazi Angelina Mabula amesema Serikali itaanza kuweka
alama za mipaka ya kimataifa katika mipaka yake na nchi jirani za Kenya na
Uganda kuanzia machi mwaka huu.
Hatua hiyo inafuatia
baadhi ya alama za mipaka yake na nchi jirani katika maeneo mbalimbali kuharibika ama kuchezewa na hivyo kuleta
mkanganyiko baina ya Tanzania na nchi hizo ni wapi mwisho wa mipaka.
Akizungumza katika
ziara yake mkoani Mara, Mabula amesema kwa sasa fedha kwa ajili ya kazi hiyo imeshatengwa
na kinachosubiriwa ni kuanza rasmi kwa kazi hiyo hapo machi mwaka 2018.
‘’katika zoezi la
kuweka alama za mipaka vitawekwa vigingi kila baada ya umbali wa mita mia moja
sambamba na kubainishwa eneo la ardhi huru’’ alisema Mabula.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, tayari timu ya wataalamu kutoka
nchi za Kenya Uganda na Tanzania zimeshakutana na kukubaliana kuhusiana zoezi
la uainishaji mipaka ya nchi hizo.
Aidha, Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema
kwa sasa alama zitawekwa katika mipaka iliyopo mikoa ya Mara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga na baadaye zoezi litaendelea katika maeneo mengine ya
mipaka.
Amesema, ni imani yake
baada ya kukamilika kwa zoezi la kuweka alama za kimataifa za mipaka suala la
migogoro kuhusiana na mipaka litakwisha.
Kwa mara ya mwisho
zoezi la kuweka alama za mipaka ya kimataifa baina ya Tanzania na nchi jirani lilifanyika
mwaka 1975 baada ya lile la awali la Tangazo la Serikali (GN) mwaka 1965
kuhusiana na mipaka.
Mkuu wa Wilaya ya
Tarime Grorious Luoga alimueleza naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kuwa, mbali na suala la mipaka ya kimataifa wilaya yake inakabiliwa na
changamoto ya mipaka baina ya hifadhi ya Serengeti na wananchi wanaozunguka
hifadhi hiyo kwani wamekuwa wakivamia na kujenga ndani ya hifadhi na wakati
mwingine kuingiza mifugo.
Katika ziara yake ya kukagua
mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la Serengeti, Naibu Waziri wa Ardhi,
nyumba na Maendeleo ya Makazi Mabula alifuatana na Mkuu wa Wikaya ya Tarime Glorious
Luoga pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Upimaji Vijijini kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Huruma Lugalla ambapo kwa pamoja walijionea hali halisi
ya mpaka wa Tanzania na Kenya na baadhi ya alama za mipaka zilizoharibika.
0 comments:
Post a Comment