Na Mwandishi Maalum- Mara
Naibu waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya
makazi Angelina mabula amezishauri halmashauri
za mji na wilaya ya Musoma mkoa wa Mara kununua nyumba zilizojengwa
na shirika la nyumba la taifa (NHC) kwa
ajili ya watumishi wake.
Mabula ametoa ushauri
huo alipotembelea nyumba hamsini zilizojengwa na shirika la nyumba la taifa
(NHC) katika eneo la Buhare katika manispaa ya
Musoma mkoani Mara.
Amesema, ni jukumu la
serikali kuhakikisha watumishi wake wanakuwa na makazi bora na rahisi kwao hasa
pale mtumishi anapohitajika kwa haraka katika kutekeleza majukumu yake.
Naibu waziri wa ardhi
nyumba na maendeleo ya makazi alisema, alitegemea halmashauri za Musoma
zingezichukua nyumba hizo zilizojengwa na shirika la nyumba kama ambavyo
imefanyika katika maeneo mengine ya Geita na Uyui.
Amezitaka halmashauri
za mji na wilaya ya Musoma kulitumia shirika la nyumba la Taifa (NHC) katika
kujenga nyumba zake pamoja na kupanga katika nyumba za shirika hilo.
Aidha, alizitaka
halmashauri kuhakikisha zinapeleka huduma muhimu kama maji na miundo mbinu
katika maeneo ambayo shirika la nyumba la taifa
linaendesha miradi yake ili kupunguza gharama za ujenzi na hivyo kuleta
unafuu wakati wa kuuza nyumba na kupanga.
Naibu Waziri wa Ardhi
nyumba na maendeleo ya makazi ameshauri
pia nyumba za shirika hilo ambazo serikali imeshindwa kuzinunua zitangazwe kwa
wananchi ili wale wenye uwezo waweze kuzinunua kwani ni nyumba bora na za
kisasa.
Naye Meneja wa Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC) Frank Mambo, amemueleza Naibu Waziri wa ardhi nyumba
na maendeleo ya makazi kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba 50 wenye lengo la
kuwapatia wananchi makazi bora ulianza mwaka 2014 na unatarajia kukamilika
Machi 2018. Amesema mradi huo unahusisha nyumba za makazi, maduka, zahanati na
maeneo ya kupumzikia.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi
22 Februari, 2018
0 comments:
Post a Comment