Na Mwandishi Maalum- Mara
Naibu waziri wa ardhi
nyumba na maendeleo ya makazi mhe. Angelina Mabula ameshangazwa na uwepo wa
majalada ya ardhi katika halmashauri za Butiama na Musoma ambayo wamiliki wake
hawafahamiki na majalada hayo kujulikana kama ‘’ndugu mhusika’’.
Akiwa katika ziara yake
ya siku tatu ya kushughulikia migogoro ya ardhi pamoja na kukagua mfumo wa
ulipaji kodi ya ardhi mkoani Mara mhe. Mabula alisema majalada hayo yamekuwa na matatizo ya viwango
vya kulipa kodi kwa kuwa yanaonekana kuwa deni huku mmiliki akitaka
kumilikishwa upya kwa gharama ndogo.
Kufuatia mkanganyiko
huo, naibu waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi aliyakabidhi majalada yenye utata kwa taasisi
ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kwa uchunguzi zaidi ili kubaini
kama suala hilo limefanyika kimakosa ama ni kwa makusudi.
‘’Mtu anamilikishwa leo
kwa pesa ndogo sana halafu za huko nyuma zinapotea hapa kuna mchezo unafanyika
kupunguza mapato ya serikali’’ alisema Mabula.
Aidha, naibu waziri wa
ardhi nyumba na maendeleo ya makazi ametaka majalada ya ardhi kuingizwa katika
mfumo kwa kila robo ya mwaka ili iwe rahisi kufuatilia waliolipa kodi ya ardhi
na wale wasiolipa.
Kwa mujibu wa Mabula
tatizo baadhi ya watumishi hawana nia thabiti ya kutumia mfumo wa kukusanya
maduhuli ya serikali ndiyo maana utekelezaji wa maagizo yanayotolewa unashindwa
kufanikiwa.
Awali mkuu wa wilaya ya
Musoma Dk. Vicent Anney Naano alimueleza naibu waziri wa ardhi nyumba na
maendeleo ya makazi kuwa wilaya yake ina changamoto kubwa ya watumishi wa
ardhi, ukosefu wa ramani za vijiji, kutoendelezwa kwa baadhi ya viwanja na
wananchi wengi kutokuwa na fedha kwa
ajili ya kupimiwa maeneo yao.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi
22 Februari, 2018
0 comments:
Post a Comment