METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 5, 2018

BUSWELU WAAZIMISHA MIAKA 41 KUZALIWA CCM KWA UJENZI WA MADARASA

Chama Cha Mapinduzi kata Buswelu, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza kimeadhimisha sherehe za kutimiza miaka 41 tangu kuzaliwa kwa chama hicho kwa kushiriki ujenzi wa madarasa matano ya shule ya msingi Bulola kama ishara ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo

Akizungumza wakati wa ujenzi huo Diwani wa Viti Malumu kata ya Buswelu  Mhe Rosemary Mwakisalu amesema kuwa wameamua kuhamasisha na kushiri zoezi la ujenzi wa madarasa hayo ili kusaidia watoto masikini na wanyonge waweze kupata elimu bora katika mazingira yanayoridhisha na kwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kutoa ELIMU BURE kama inavyoelekeza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi,  Na hao kama  wananchama kuamua kutumia sherehe hizo za kutimiza miaka 41 kwa kufanikisha ujenzi huo

‘… Tumeamua kuhamasishana na kushiriki zoezi la ujenzi  wa madarasa matano kwa shule hii ya Bulola kuunga mkono Sera ya ELIMU BURE ya Serikali yetu na viongozi wetu kama unavyojua HAPA NI KAZI TU na TUKUTANE KAZINI, Hivyo kwa kuadhimisha miaka 41 ya kuzaliwa kwa Chama Chetu Cha Mapinduzi tukaona tujumuike pamoja kuisaidia shule hii yenye upungufu wa madarasa …’ Alisema

Aidha Mhe Rosemary Mwakisalu amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa msaada wake wa tofali 1500  alizozitoa kwaajili ya ujenzi huo  na mpango wake wakuhimiza maendeleo kwa kata zote za Jimbo lake kwa kuwataka wananchi kuanzisha misingi  ya ujenzi wa majengo ya huduma za jamii  na yeye kumalizia panapobaki akishirikiana na halmashauri ya manispaa ya Ilemela

Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Kata ya Buswelu Komredi  Lugalata Daud amefafanua kuwa msingi wa chama chake ni watu wanyonge na masikini  hivyo chama chake kitaendelea kusaidia utatuzi wa changamoto na kero zinazowakabili wananchi wake kama ambavyo kimefanya kwa shule hiyo yenye upungufu wa madarasa baada ya ongezeko la  wanafunzi lililochangiwa na  Sera ya Elimu Bure.

Akihitimisha Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Ndugu Malipesa Elias ameshukuru kwa uamuzi uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi kata ya Buswelu kwa kuja kwenye shule anayoiongoza kuhamasiha na  kushiriki ujenzi huku akisisitiza kuwa suala la maendeleo halina itikadi ya vyama vya siasa, dini wala kabila hivyo ni jukumu la kila mwananchi kushiriki na kuunga mkono shughuli za maendeleo kwani wanaonufaika ni jamii nzima

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com