Chama Cha Mapinduzi kata Buswelu, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza kimeadhimisha sherehe za kutimiza miaka 41 tangu kuzaliwa kwa chama hicho kwa kushiriki ujenzi wa madarasa matano ya shule ya msingi Bulola kama ishara ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo
Akizungumza wakati wa ujenzi huo Diwani wa Viti Malumu kata ya Buswelu Mhe Rosemary Mwakisalu amesema kuwa wameamua kuhamasisha na kushiri zoezi la ujenzi wa madarasa hayo ili kusaidia watoto masikini na wanyonge waweze kupata elimu bora katika mazingira yanayoridhisha na kwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kutoa ELIMU BURE kama inavyoelekeza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, Na hao kama wananchama kuamua kutumia sherehe hizo za kutimiza miaka 41 kwa kufanikisha ujenzi huo
‘… Tumeamua kuhamasishana na kushiriki zoezi la ujenzi wa madarasa matano kwa shule hii ya Bulola kuunga mkono Sera ya ELIMU BURE ya Serikali yetu na viongozi wetu kama unavyojua HAPA NI KAZI TU na TUKUTANE KAZINI, Hivyo kwa kuadhimisha miaka 41 ya kuzaliwa kwa Chama Chetu Cha Mapinduzi tukaona tujumuike pamoja kuisaidia shule hii yenye upungufu wa madarasa …’ Alisema
Aidha Mhe Rosemary Mwakisalu amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa msaada wake wa tofali 1500 alizozitoa kwaajili ya ujenzi huo na mpango wake wakuhimiza maendeleo kwa kata zote za Jimbo lake kwa kuwataka wananchi kuanzisha misingi ya ujenzi wa majengo ya huduma za jamii na yeye kumalizia panapobaki akishirikiana na halmashauri ya manispaa ya Ilemela
Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Kata ya Buswelu Komredi Lugalata Daud amefafanua kuwa msingi wa chama chake ni watu wanyonge na masikini hivyo chama chake kitaendelea kusaidia utatuzi wa changamoto na kero zinazowakabili wananchi wake kama ambavyo kimefanya kwa shule hiyo yenye upungufu wa madarasa baada ya ongezeko la wanafunzi lililochangiwa na Sera ya Elimu Bure.
Akihitimisha Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Ndugu Malipesa Elias ameshukuru kwa uamuzi uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi kata ya Buswelu kwa kuja kwenye shule anayoiongoza kuhamasiha na kushiriki ujenzi huku akisisitiza kuwa suala la maendeleo halina itikadi ya vyama vya siasa, dini wala kabila hivyo ni jukumu la kila mwananchi kushiriki na kuunga mkono shughuli za maendeleo kwani wanaonufaika ni jamii nzima
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '
No comments:
Post a Comment