
Na BMG
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile ametembelea hospitali ya Rufaa Kanda ya Ziwa Bugando
iliyopo Jijini Mwanza ili kujionea namna shughuli mbalimbali za afya
zinafanyika hospitalini hapo.
Dkt.Ndugulile
alifanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo jana na kubainisha kwamba
kati ya akina mama 100,000 wanaojifungua nchini, akina mama 556 hupoteza
maisha na kwamba ili kupambana na changamoto hiyo, serikali imeweka
mkakati wa kuboresha zaidi utoaji huduma za afya katika Vituo vya afya
kote nchini.
"Kanda
ya Ziwa ina vifo vingi vinavyotokana na kujifungua hivyo kuboresha
vituo vya afya ni moja ya mikakati ya serikali katika kupunguza vifo
hivyo kwa kujenga vyumba vya upasuaji, wodi ya akina mama na mtoto,
maabara, kitengo cha dharura pamoja na kuweka gari la wagonjwa
(Ambulance) litakalosaidia kumfikisha mgonjwa kupata huduma haraka".
Alisema Dkt.Ndugulile.
Alisema
serikali inafahamu changamoto ya upungufu wa rasirimali watu katika
afya hivyo itaendelea kusomesha madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali
ambao watafanya kazi kwa kufuata maelekezo yake li wananchi wa maeneo
husika wapate huduma bila kulalamika.
Pia
alisema serikali itaendelea kuboresha huduma za afya mahospitalini ili
kuweka mfumo vizuri wa rufaa kwa kila ngazi ya hospitali kufanya kazi
kulingana na nafasi yake kama vituo vya afya, zahanati, hospitali za
wilaya, mkoa rufaa kanda na taifa.
Aidha
alisema rufaa za wagonjwa nchini zimepungua kwani kwa sasa kuna taasisi
zenye zinauwezo wa kutoa huduma ya matibabu ya magonjwa ya upasuaji
mifupa na kansa ambayo ndio magonjwa yaliyosababisha wagonjwa wengi
kutibiwa nje ya nchi na kwamba hivi sasa kuna wagonjwa nje ya nchi
ikiwemo Uganda hupata rufaa kutibiwa hapa nchini.
Mkurugenzi
Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt.Abel Makubi
alimshukuru Naibu Waziri Dkt.Ndungulile kwa kutembelea hospitali hiyo na
kwamba aliyoshauri yatafanyiwa kazi.
Dkt.Makubi
aliishukuru wizara ya afya kwa kutoa shilingi milioni 420 kwa ajili ya
dawa za kansa ambazo hapo awali zilikua changamoto kwa wagonjwa wengi
pamoja na kusaidia ujenzi wa jengo la kitengo cha kansa ambapo awamu ya
kwanza imekamilika na inasubiriwa ujenzi wa awamu ya pili ya wodi.
0 comments:
Post a Comment