Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wametakiwa kutowafumbia macho Viongozi wanaoshirikiana na Wataalamu katika kuhujumu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali yao
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM kwa kata ya Nyamhongolo na Nyakato kueleza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ambapo amefafanua juu ya mambo aliyoyafanya kwa kipindi cha miaka miwili katika eneo lao ikiwa ni ujenzi wa Matundu 12 ya Vyoo, Ujenzi wa madarasa 3 na Madawati 160 kwa shule ya msingi Ibeshi, Ugawaji wa Mifuko 70 ya Saruji na tofali 4750 za ujenzi wa Zahanati ya Nyamadoke, Ujenzi wa gati 7 za Maji, Ujenzi na ufunguzi wa kisima cha maji kinachotumia nishati ya Jua Nyamadoke, Ugawaji wa Vitabu vya Sayansi na utoaji wa elimu ya Ujasiriamali kwa vikundi 34 huku akiwataka kuwaumbua na kuwachukulia hatua wale wote wanaohujumu na kukwamisha miradi ya maendeleo
‘… Mnatakiwa kuwa macho kwenye miradi inayotumia fedha za Umma na msione aibu kusema kwa maana ya nyinyi ambao mmetupa dhamana sisi ya kuitekeleza Ilani, Kuna wengine wahandisi humu hata kama hamfanyi kazi si mnaona miradi ya chini ya kiwango sasa lazima kutoa taarifa kwa kumwambia mhusiaka palepale…’ Alisema
Aidha Mhe Mbunge ameshukuru na ametaja mafanikio na miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe Rais Dkt John Magufuli ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa viwanda, ujenzi wa reli ya kisasa, utoaji elimu bure, urasimishaji makazi na upangaji miji kupitia wizara ya Ardhi zoezi litakalofika ukomo mwezi Juni 30 mwaka huu, upanuzi wa uwanja wa ndege, ongezeko la ukusanyaji wa mapato, ongezeko la bajeti ya afya vitu ambavyo vitamsaidia Mtanzania kutoka kwenye umasikini sambamba na kuufanya mkoa wa Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika ya Mashariki hivyo kuwataka wananchi wake kuitumia vizuri fursa hiyo
Kwa upande wake Muwakilishi wa Uongozi wa CCM wilaya ya Ilemela aliyeambatana na Mbunge huyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa wilaya Ndugu Denis Lekela Kankono mbali na kupongeza jitihada za utekelezaji wa Ilani ametaka kuchukuliwa hatua kwa watendaji wote wa Serikali wasiokuwa waadirifu huku akiomba wanachama kuendelea kuunga mkono na kutangaza mema yanayofanywa na Serikali yao
‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
14.01.2018
0 comments:
Post a Comment