NA PAUL WILIUM, MOSHI.
*@Million Media Group*
*_MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro, Daudi Mrindoko amewataka Wananchi wote waliovamia maeneo ya shule za Jumiya hiyo na kujenga makazi ya kudumu kuondoa makazi hayo kwa hiari yao wenyewe kabla ya sheria hazijachukuliwa_*.
Kauli hiyo aliitoa leo wakati wa ziara katika shule ya Kibo sekondari iliyopo manispaa ya Moshi inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ambapo alikutana na Bodi ya shule na kuongea nayo.
Mrindoko alisema kuwa, shule hiyo ya Kibo ilikuwa na eneo lenye ukubwa wa hekari 20, lakini katika hali ya kushangaza Wananchi wamevamia na kujenga makazi yaliyopelekea shule hiyo kubakiwa na hekari 15.
*"Wapo baadhi ya watu wamevamia maeneo ya shule zetu na kujenga makazi hayo lakini niwaagize waanze kuondoa wenyewe makazi yao kabla ya sheria kuchukuliwa, Mwenyekiti wa ccm Taifa, Dkt. John Pombe Magufuli ameunda tume ya kuchunguza mali za chama kabla tume hiyo haijafika Kilimanjaro mimi nataka nishughulike na hawa waliovamia maeneo yetu” alisema Mrindoko*.
Alisema kuwa, katika kipindi chake cha miaka mitano ya uongozi wa Jumuiya hiyo mkoa atahakikisha kuwa miradi yote ya Jumuiya inakuwa salama huku akiwatupia lawama wapimaji wa Ardhi Manispaa ya Moshi, kwa kuwatengenezea hati Wananchi wanaovamia maeneo yanayomilikiwa na Jumuiya hiyo kihalali.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa, shule ya Sekondari ya Kibo ni miongoni mwa shule za Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mitihani ya Taifa lakini imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa Wanafunzi.
Alisema kuwa, Majengo yote ya Jumuiya hiyo yasiyotumiwa katika shule ya Sekondari ya Kibo watayakodisha kwa Wawekezaji ili waweze kufungua shule ya Awali na Msingi ili pindi wanafunzi hao watakapohitimu elimu yao ya msingi waweze kujiunga na shule ya Sekondari ya Kibo.
“Tunayo maeneo makubwa ambayo hatuyatumii hivyo nitumie fursa hii kuwatangazia Wananchi wanaotaka kuwekeza kufika katika ofisi zetu za Jumuiya ili tuweze kuingia mkataba wa kuwekeza na kuweza kuisaidia Jumuiya na shule zetu kupata kipato cha kujiendesha” alisema Mrindoko.
Kwa upande wake, Katibu wa Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, Hatibu Mnuwa alisema kuwa, wapo baadhi ya watu walipendekeza kuuzwa kwa shule hiyo lakini Wanachama wa CCM wanaozunguka shule hiyo walipinga kuuzwa kwa shule hiyo kutokana na kutambua kuwa eneo la shule hiyo ni kitega uchumi kizuri kutokana na kuwa mjini.
Mnuwa alisema kuwa, shule hiyo kwa sasa imeshindwa kujiendesha kutokana na kuwa na mzigo mkubwa wa madeni yaliyosababishwa huko nyuma na bodi huku pia akidai kuwa sababu nyingine ni kutokana na shule hiyo kukosa kitenga uchumi cha kuiingizia mapato.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo ya Kibo, Charles Shilindealisema kuwa, lengo la walimu katika shule hiyo ni kuhakikisha ufauli wa Wanafunzi katika shule hiyo unakuwa ili kuwavutia wazazi kuwapeleka Watoto wao katika shule hiyo.
Alisema kuwa, changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni upatikanaji wa Wanafunzi kutokana na Wanafunzi wengi wanaohitimu elimu ya msingi hujiunga na shule za Sekondari za Serikali na hii imesababishwa na ada kuwa bure katika shule hizo.
Aidha mkuu huyo wa Shule ameiomba Serikali kuzuangalia shule za binafsi kwani zinafanya kazi moja ya kuelimisha Taifa la Tanzania na kuzipatia ruzuku shule hizo.
Mwisho………..
15/01/2018
0 comments:
Post a Comment