Na Mathias Canal, Wazohuru.com
Kaimu Mkuu Wa Wilaya ya Dodoma ambaye pia ni Mkuu Wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deogratius Ndejembi Leo 27 Januari 2018 ametembelea eneo lililoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani humo kujionea jinsi ambavyo wananchi wamekumbwa na adha kwa kushindwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Mhe Ndejembi amejionea namna ambavyo wananchi wamekumbwa na kadhia hiyo katika eneo La Chang'ombe ambapo ametilia msisitizo wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi kifupi ambacho serikali inaharakisha namna bora ya kuimarisha usalama wao na kuondoa maji yaliyotuama katika maeneo hayo ya makazi.
Akizungumza na wakazi Wa maeneo hayo Mhe Ndejembi ameuagiza uongozi. Wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kutembelea eneo hilo kabla ya jua kuzama ili kujionea kadhia hiyo na kuona namna ya kuelekeza maji hayo maeneo yapotakiwa kuelekea ili kunusuru mlundikano huo Wa maji ambao umeanza kuathiri wakazi Wa maeneo hayo kwa kubomoka kwa nyumba.
Aidha, alisema kuwa kutokana na mvua hiyo baadhi ya vyoo vimeanza kufumuka na kutoa uchafu jambo ambalo ni athari kwa afya za wananchi Wa maeneo hayo ya Chang'ombe.
Katika hatua nyingine Mhe Ndejembi amemuagiza pia Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma kupeleka wataalamu wa ardhi ili kuangalia nyumba zilizojengwa kinyume na taratibu na kuziba barabara jambo linalopelekea maji kukosa uelekeo na hatimaye kutuama katika maeneo ya makazi.
Awali Kaimu Mkuu huyo Wa Wilaya ya Dodoma alishuriki zoezi la usafi na wananchi ambapo Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo alisikiliza kero za wananchi huku kadhia mbalimbali serikali ikiwa mbioni kuzitatua.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment