METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, January 4, 2018

MBUNGE WA ILEMELA AFUNGA MASHINDANO YA KIRUMBA SUPER CUP 2017

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amefunga mashindano ya ligi ya mpira wa miguu iliyohusisha Timu Saba kutoka Mitaa ya Kata ya Kirumba iliyojulikana kama KIRUMBA SUPER CUP 2017 na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa Comred Kheri James, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Kirumba na Diwani wa Kata hiyo Mhe Alex Ngusa

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia fainali ya mashindani hayo iliyochezwa  katika Uwanja wa Magomeni kata ya Kirumba ikihusisha Timu ya MKOKOTENI FC na JURA FC Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kuelezea historia ya Kata ya Kirumba katika kuzalisha wachezaji nguli na tegemezi kwa vilabu mbalimbali vya soka nchini amewahakikishia kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha anakuza vipaji vya vijana ndani ya jimbo lake kupitia mashindano ya  JIMBO CUP yanayofanyika kila mwaka huku akisisitiza faida za michezo kwa jamii

‘… Kwa hiyo unapocheza hapa huchezi kujifurahisha ni lazima mtambue kuwa michezo ni afya michezo ni ajira, mbali na timu kubwa  zinazopita kuwatazama ili kuibua vipaji vipya nyie wenyewe mtakuwa mmejikinga na maradhi mbalimbali …’ Alisema

Aidha Mhe Dkt Angeline  Mabula ameongeza kuwa mshindi wa mashindano hayo atapata fursa ya kushiriki mashindano ya JIMBO  CUP mwaka  huu wa 2018 yanayotarajiwa kuanza muda si mrefu sana kutoka sasa

Kwa upande wake muendeshaji wa mashindano hayo Ndugu Mohamedi Rajabu amesema kuwa lengo la kuandaa mashindano hayo ni kuwakutanisha watu karibu na kuibua vipaji vipya huku ikiwasaidia vijana kutojiingiza katika mambo yasiyofaa ikiwemo uvutaji bangi na matumizi ya madawa ya kulevya

Fainali hiyo iliisha kwa Timu ya MKOKOTENI FC kuichapa Timu ya JURA FC goli moja kwa sifuri, Goli lililofungwa dakika ya 38 kipindi cha kwanza na mchezaji machachari Liberatus Mgeta na kuifanya timu yake kuibuka kidedea na kujinyakuria Ng’ombe mnyama mmoja, Kombe na Jezi seti moja zawadi iliyokabidhiwa na mgeni rasmi Dkt Angeline Mabula huku  Mwenyekiti wa Vijana UVCCM Taifa Kheri James akikabidhi Mbuzi mnyama na mpira kwa mshindi wa pili Timu ya JURA FC

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane ’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
04.01.2018

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com