Na WMJJWM- Mara
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa siku thelathini kwa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kuunda Madawati ya Kijinsia katika vyuo vyao.
Dkt. Gwajima, ameyasema hayo wakati wa ziara yake kwenye Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Buhare kilichopo Mkoani Mara, ambacho ni miongoni mwa Vyuo ambavyo havijaanzisha madawati hayo.
“Ndani ya siku hizi thelathini Madawati haya yawe yameanzishwa katika Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, haikubaliki kuona ninyi mnaosimamia Maendeleo ya Jamii mshindwe kuwa na Dawati husika” alisema Dkt. Gwajima.
Akiongea kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara Bi Neema Ibamba, amesema wamezingatia maagizo ya Wizara na atayafikisha kwa Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Chuo watayafanyia kazi kwa kushirikiana na Chuo kutekeleza maelekezo hayo.
Kwa Upande wake rais wa Serikali ya Wanafunzi Feleki Alek, ameiomba Serikali kuona haja ya kuanzishwa kwa kozi za Shahada katika Chuo hicho itakayokipa hadhi Chuo katika kutengeneza wataalam wa Maendeleo ya Jamii nchini.
“Katika Mkoa wetu wa Mara hatuna Chuo chenye kutoa Shahada, hivyo kama Mwakilishi wa Serikali ya Wanafunzi na kutokana na ukongwe wa Chuo hiki, kwanza tunaomba Majengo yaongezwe lakini pili, tunaomba Chuo kipewe hadhi ya kutoa Degree” alisema Felik.
Awali akitoa Salaam za Chuo, Mkuu wa Chuo hicho Paschal Mainyila, alisema Chuo hicho kilianzishwa mwaka 1966 na kwa sasa kinatoa kozi za ngazi ya Stashada na Astashahada na kinaendelea na jitihada za kuhakikisha kinazalisha wataal wa Maendeleo ya Jamii watakaosaidia kubadili fikra katika jamii katika kutataua changamoto mbalimbali katika jamii.
Wakati huo huo Waziri Dkt. Gwajima amekutana na Viongozi wa wamachinga Mkoa wa Mara na kuzungumza nao kuhusu changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.
Dkt. Gwajima amesema, masuala ya changamoto za Machinga ikiwepo kuhamahama, watazungumza na Mamlaka za Mikoa ili kuona namna Bora ya kutatua tatizo hilo, na hii itakuwa ni kwa nchi nzima.
“Machinga wasingekuwepo hivi mahitaji ya haraka haraka tungekuwa tunapata wapi? Hivyo kama Serikali tunathamini sana uwepo wenu” alisema Dkt. Gwajima
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Mara, Charles Waitara, ameiomba Serikali kuendelea kuliratibu kundi hilo ili liweze kufanya shughuli katika mazingira wezeshi.
“Mhe. Waziri sisi tunakuwa waanzilishi wa eneo, lakini likishachangamka tunaondolewa, hii kwakweli inanyong’onyeza jitihada zetu, tunaimani chini ya Uongozi wako hili halitajitokeza” alisema Waitara.
0 comments:
Post a Comment