Mradi wa majaribio wa miezi 15 wa watoto waliokosa shule, kujifunza wenyewe kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayotumia tableti umezinduliwa mkoani Tanga.
Mradi huo uliozinduliwa katika kijiji cha Zenith ya Kati, wilayani Muheza ni sehemu ya mradi mkubwa wa miaka mitano wa majaribio duniani chini ya Global Learning Xprize wenye lengo la kutatua matatizo ya kujifunza.
Mradi huo hapa nchini unaendeshwa kwa pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na XPrize ambao wametoa tableti husika.
Aidha kuwezekana kuwapo kwa mradi huo kumetokana pia na makubaliano kati ya serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake ya elimu na TAMISEMI na mashirika.
Katika utoaji elimu huo watoto wanaohusika ni wa miaka kuanzia 9 hadi 11 na watajifunza kwa kutumia program tano zilizowekwa katika tableti zitakazomuwezesha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mradi huo wa Tanga ambao utagusa watoto 2,400 kutoka katika vijiji 167 vya wilaya za Handeni, Korogwe, Lushoto, Muheza, Mkinga na Pangani unatoa changamoto kwa timu ya wabunifu kuwezesha watoto walio na fursa ndogo ya kuingia katika elimu darasani kujifunza stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kutumia tableti wakijifunza wenyewe.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo katika kijiji cha Zenith, Muheza Mkoani Tanga, Mwakilishi wa Unesco ambaye pia anasimamia mradi huo Faith Shayo alisema kwamba mradi huo unaendana na majukumu ya Unesco ya kuhamasisha elimu jumuishi katika kuhakikisha kwamba watoto wote wa Tanzania wakiwemo wa jamii za pembezoni zilizo nyonge zinapata fursa.
Alisema UNESCO inatekeleza majukumu yake kwa kuisaidia serikali ya Tanzania kuwezesha kutoa elimu bora kwa wananchi wake wote na hata wale ambao hawana uwezo wa kupata elimu kutokana na mazingira yao au maeneo yao.
Alisema Unesco kwa kuangalia mahitaji imekuwa ikisaidia serikali ya Tanzania katika vitu mbalimbali vya kiufundi ili iweze kufanikisha lengo la kuwa na taifa la watu walioelimika hivyo kuwa na nafasi ya kushiriki katika kazi za kujenga uchumi.
“Mradi huu unawapa watoto ambao hawakuwahi kujiunga na shule ya msingi, fursa nyingine”alisema Faith na kuongeza kwamba juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa utaimarisha viwango vya weledi nchini.
Faith anasema kwamba kwa sasa japo upo kwenye majaribio utakapofanikiwa utaweza kufanyiwa kazi maeneo mengine ya Tanzania.
Aidha Mwakilishi wa WFP mkoa wa Tanga ambaye ndiye anayesimamia utekelezaji wa programu hiyo, Xavery Njovu alisema kwamba watoto hao wataangaliwa kwa namna ambavyo wanaelewa kila wiki, wanapoenda kuchaji tableti zao.
“wakati wa kuchaji pia tunaangalia matumizi ya tableti na ufaulu wa mtoto katika kumaliza porogramu utaonekana na kama ikionekana hasongi mbele itaangaliwa kasoro” alisema Njovu.
Alisema kuna vijana 10 wanaojua Tehama na wamefundishwa kusaidia wanafunzi hao katika kuhakikisha kwamba tableti hazikwami au kuharibika. Watu hao wanaoishi vijijini hukohuko pamoja na kulipwa mishahara wamepewa pikipiki mpya aina ya Yamaha kwa lengo la kuhakikisha wanafika kila kata yenye wahusika na kuzungumza nao.
Pamoja na tableti hizo pia kumefungwa sola za kuchajia na seva ya kuangalia mwenendo wa watumiaji wa tableti.
Kabla ya kuzinduliwa kwa mradi huo watu 282 walifunza namna ya kuhudumia vijana hao ambao wanashiriki katika program.
Katika mafunzo hayo wasimamizi hao ambao wanajulikana kama mama au baba vitongoji walifunza malengo ya mradi na namna ya kuangalia mwenendo wa watoto na mradi wenyewe.
Mgeni rasmi katika ukabidhiaji wa tableti, Ofisa Elimu wa mkoa wa Tanga, Mayasa Hashimu aliwataka wazazi kuhakikisha kwamba tableti hizo zinatumiwa na watoto kwa makusudi yaliyopangwa ili kuwa na taifa la watoto wenye weledi mkubwa.
Alisema tableti hizo maalumu ni msaada mkubwa kwa wananchi na serikali hivyo hawana budi kuzitunza na kuzitumia kwa makusudio husika.
“teknolojia hii inayowezesha watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu pasipo msaada wa mwalimu ni ubunifu wa kiwango cha juu kabisa” alisema Mayasa na kuongeza kwamba hali hiyo itabadili kabisa fikra za utoaji elimu na kuwakomboa watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Aliwataka wazazi kuunga mkono jitihada za serikali kupitia kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kusaidia kujenga taifa lenye uelewa mkubwa kupitia chanzo cha sasa cha maarifa pasipo msaada wa mwalimu darasani.
Alisema msaada huo ni pamoja na kutunza vifaa vyote vya mradi na kutumiwa na wahusika bila kukosa.
Aidha alishukuru Shirika la UNESCO, XPRIZE na WFP kwa kuonesha njia na kusema kwamba mkoa utafanya kila linalowezekana kuona mradi huo wa majaribio unafanikiwa.
Katika makadihiano hayo watoto zaidi ya 10 walipewa tableti kwa niaba ya wenzao ambao wanashiriki katika mradi.
Mmoja wa wazazi wa watoto waliokabidhiwa tableti aliyejitambulisha kwa jina la Musa Ramadhani alisema amefurahishwa sana na mpango huo na kuahidi kuhakikisha kwamba anatunza kifaa hicho ili mtoto wake afaidike nacho.
“Mtoto wangu mimi anaitwa Amir Musa na ana miaka 9; hapa tulipo ni ndani sana kupatiwa kifaa hicho kitatusaidia sisi maskini tuliosahaulika kuwa katika utaratibu tena wa weledi”alisema.
Aidha alisema kwamba dhamana ya utunzaji inamuangukia yeye kwa kuwa anaamini ni kazi yake kuhakikisha kwamba mtoto wake anapata mafanikio kutokana na mradi huo.
Naye mama Kitongoji Hilda Hule alisema kwamba ana uhakika kwamba watoto hao watapata maarifa na kujua kusoma kwa kasi zaidi kwa kuwa hatua za mwanzo zilionesha hamu yao ya kutaka kujua.
Anasema kwa upande wake yeye anawaangalia watu wa kitongoji cha Zeneth na anaamini kwamba kwa mradi huo watoto wengi watafunguka.
Mmoja wa mateknisheni wa mradi huo ambao watasaidia uwapo wa tableti na program zake Francis Kibaja mwenye makazi yake Korogwe alisema kwamba mfumo huo wa kitabu cha kielektroniki kinamfanya mwanafunzi ajifunze na kujisahihisha na kama watamaliza programu mapema kutokana labda kwa urahisi watawapangia programu ngumu zaidi ili kuwakomaza.
Aidha alisema kwamba tableti hizo zinagemu kwa ajili ya mtoto akichoka na pia wakati wa mazoezi program itamwambie mtoto kama amekosea au amepatia.
Programu zilizowekwa kwa sasa katika tableti hizo ambazo hazina uwezo wa simu ni sawa na mtu kuanza darasa la awali na kuingia shule ya msingi.
Katika mradi huo WFP wamepewa dhamana ya kusimamia uendeshaji wa kitengo cha lojistiki na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama-ICT) cha majaribio katika mazingira halisi.
Aidha jukumu lake ni pamoja na kuingiza programu katika tableti, kuanzia vituo vya kuwekea umeme unaotokana na jua kwenye tableti hizo vijijini, kusimamia matengenezo, marekebisho na kutoa tableti mpya kipindi chote cha majaribio.
Uzinduzi huo ulipambwa na mambo mbalimbali ukiwemo muziki wa asili ambapo kikundi cha JAHAZI ASILI zilitumbuiza kwa ngoma za asili za wakazi wa Tanga na pia muziki wa singeli.
Ofisa wa Xprize naye alitumbukia katika burudani za singeli na kuwa burudani kubwa kwa watu ambao walienda naye sambamba na kama yeye alivyokuwa akienda sambamba na wenyeji katika zungusha.
0 comments:
Post a Comment