METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 18, 2017

WAZEE WADAI KUKATWA FEDHA ZA MATIBABU CHEMBA

index 

Na Mahmoud Ahmad Chemba

Wazee wilayani Chemba wameilalamikia serikali kwa kushindwa kuwahakiki ili waweze kupata huduma ya matibabu bure kwa kutoanzishwa kwa mabaraza ya wazee kuanzia ngazi ya Kijiji kata hadi wilaya ambapo pia wenzao ambao hawana kaya wapo pekee yao wamekuwa wakikatwa fedha za Tasaf kiasi cha tsh.13,000 kwa ajili ya kuagharimia matibabu.

Akizungumza na wanahabari mmoja ya wazee Iddy Kidangi (87) amesema kuwa kero yao kubwa ni kukatwa fedha zao zinazotokana na mradi wa Tasaf wa kuzisaidia kaya masikini lakini wamekuwa wakishangaa serikali ikiendelea kusema kuwa huduma ya matibabu kwa wazee ni bure hapa wanatusaidia kweli alihoji.

Amesema kuwa hadi sasa hawajaona mpango wowote ulioandaliwa wa kuwajua wazee wanaotakiwa kupata huduma ya matibabu bure katika maeneo yao licha ya wao kupeleka taarifa za uwepo jambo linalowawia vigumu wakati wanapofika kwenye vituo vya afya kupata huduma kukosa ushirikiano na wahudumu na mda mwingine kukosa hata matibabu mpaka watoe pesa.

“Hakuna mpango  wa kuwasajili wazee wanaongia kwenye uzee wala kujua idadi yao tunaiomba serikali kufika maeneo ya vijijini kuona hali hiyo na kuweza kuwapatia msaada wa kupata huduma ya Afya” alisema Kidangi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Goima Bakari Jengu alisema halmashauri ina mpango wa kuhakiki wazee wote waliopo kwenye wilaya hiyo ili waweze kupanga mipango ya maendeleo na kubwa likiwa kuwasaidia wazee kupata matibabu

Amesema kuwa suala la kaya maskini ambazo hazina familia hilo hawezi kulitolea ufafanuzi na kuwataka kumtafuta mtendaji wa kata hiyo kuweza kujibu suala hilo ambapo aliongeza kuwa licha ya kuombwa katika mkutano huo wa kijiji na wazee hao kuwasaidia kupata huduma ya matibabu bure kama ilivyo sera ya serikali.

“Unajua ndugu wanahabari mkutano wetu wa kijiji tulikuwa tunazungumzia juu ya kujenga miundo mbunu ya maji ambayo iliibiwa siku za karibu na ujenzi utaanza jumatatu hivyo tunawaomba wananchi wawe na subira kwa sasa wakati tukiendelea na umaliziaji wa mradi huu wa maji” alisema Jengu

Halmashauri ipo mbioni kuwaundia mabaraza yao kuanzia ngazi ya wilaya hadi kitongoji ikiwa ni utekelezaji wa sera ya serikali kila mzee kupata huduma ya matibabu bure hivyo wazee kote nchini wametakiwa kuwa nasubira wakati mikakati hiyo ikiendelea.

Kero ya kukatwa kwa fedha za wazee waliopo kwenye mradi wa Tasaf wa kaya maskini umeonekana maeneo mengi huko vijijini bado elimu inahitajika kwa watendaji wa vituo vya afya na wanachi sanjari na watendaji wa vijiji na vitongoji ili kuondoa dhana ya wazee wenye kaya kuona fedha wanazokatwa kwa ajili ya ulipaji wa CHF kwa kaya zao sio ulaji bali ni taratibu na kanuni.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com