METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 18, 2017

ZANZIBAR KUJENGA JENGO JIPYA LA UWANJA WA NDEGE

01
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar  Dkt. Khalid Salum Mohamed akitowa taarifa kwa Waandishi wa habari juu ya Ujenzi wa Jengo jipya la Uwanja wa Ndege unaotarajiwa kuanza Desemba mwaka huu chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Mkutano huo umefanyika Ukumbi wa Wizara ya Fedha Vuga Mjini Zanzibar.
02
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Balozi Ali Karume akielezea juu ya Mradi wa  Ujenzi wa Jengo jipya la Uwanja wa Ndege linalotarajiwa kujengwa Desemba mwaka huu  ambapo unatarajiwa kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa kwa wakati uliopangwa.
03
Wandishi wa Habar wakifuatilia Mkutano wa Mawaziri 2 Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar  Dkt. Khalid Salum Mohamed na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali Karume   juu ya Ujenzi wa Jengo jipya la Uwanja wa Ndege linalotarajiwa kuanza tena Desemba mwaka huu.Picha na Maryam Kidiko wa Habari Maelezo Zanzibar.
………………………………………………………….
Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar

Waziri wa Fedha na  Mipango Dkt Khalid Salum Mohamed alisema ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege unatarajiwa kuanza tena  Disemba Mwaka huu chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  kupitia Exim Bank.

Alisema ujenzi wa  jengo jipya ni miongoni mwa miradi  mitatu mikubwa ya maendeleo katika kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume kiliopo Kisauni ambacho kinaumuhimu mkubwa kwa uchumi wa  Zanzibar. 

Hayo aliyasema katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Vuga wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu changamoto zilizojitokeza ambazo zilisababisha kushindwa kukamilika ujenzi huo .

Alisema kutokamilika kwa muda mrefu jengo jipya la kuhudumia abiria kulipelekea changamoto ya kumudu kuhudumia ndege kubwa aina ya Code E kulingana na mahitaji ya sasa na uwezo wake wa idadi ya abiria wataohudumiwa kwa mwaka .

Aidha alisema utengenezaji wa jengo kuligana na mahitaji mapya ya shirika la usafiri wa anga la duniani (ICAO) na mkabala wake wa maeneo ya kuegesha ndege yaliojengwa kwa ufadhili wa benki ya dunia .

Alieleza kutokana na kadhia hiyo Serikali ililazimika  kuajiri mshauri maalumu kutoka kampuni ADPi kutoka ufaransa ili kuweza kuishauri vizuri juu ya utatuzi wa changamoto zilizobainika  .

Hata hivyo alisema marekebisho yaliyopendekezwa na kukubaliwa na Serikali yalipelekea kuongezeka kwa gharama za mradi kutoka dola 70.4 millioni hadi 128.7 million .

Alieleza gharama hiyo ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo lenyewe eneo Zaidi la maegesho ya ndege la mita za mraba 38,000 na eneo la kuegesha gari za watumiaji wa uwanja ,abiria pamoja na wapokeaji abiria .

Waziri wa fedha alisema tatizo hasa lililojitokeza ni upatikanaji wa fedha za ziada ambapo awali Benki ya Exim ilitaka atafutwe mfadhili mwengine kwa kiasi hichi lakini baada ya mashauriano ya muda mrefu baina ya  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja  na Serikali ya Watu wa China hatimae walikubaliana kudhamini kwa mkopo wa kibiashara .

Alifahamisha kuwa kutokana  na jitihada kubwa za  Serikali na Rais wa Zanzibar  Dkt Ali Mohamed Shein Benki ya Exim ilikubali kudhamini mkopo wote wa kugharamia ujenzi huo kwa utaratibu wa mkopo nafuu.

“Benki ya Exim kwa sasa imekubali kudhamini gharama zote za dola 128.7 million kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwa masharti ya  mkopo nafuu .“alisema Waziri .

Alifafanua kuwa tayari wiki hii Benki hiyo imeshamlipa mkandarasi madai yake ya dola 17.6 millioni kwa kazi ambazo ameshazifanya awali na kuidhinishwa na mshauri dola nyengine 17.6 millioni kwa kazi kama hizo lakini zenye dhamana mpya ya mkandarasi na tayari mkandarasi amelipwa jumla ya dola 35.2 millioni .

Nae Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji  Balozi Ali  Karume alisema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa kwa wakati uliopangwa kwa muda wa miezi 18 hadi 20.

Aidha alisema Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano itahakikisha inasimamia vizuri ujenzi huo na kuhakikisha inatatua matatizo madogo madogo yatakayojitokeza ili  lengo la serikali la kuhakikisha jengo hilo jipya la abiria linauwezo wa kuchukua abiria 1,
200,000 mpaka 1,600,00 kwa mwaka .

Hata hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kuwashukuru Wananchi wa eneo la Chukwani   kwa ustahamilivu wao na imani yao kwa muda wote wakati serikali ikilitafutia ufumbuzi suala la mradi huo
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com