Frank Mvungi- Maelezo , Dodoma
Serikali imesema itaendelea
Kupanua wigo wa Upatikanaji wa huduma za Matibabu kwa wagonjwa wenye
saratani ili Kupunguza msongamano katika Hosipitali ya Ocean Road Jijini
Dar es Salaam.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalum Mhe. Leah Komanya Bungeni kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo
ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto , Waziri wa Mali Asili na Utalii Dkt.
Hamis Kigwangala amesema kuwa Serikali inakamilisha maandalizi ya
kuanzisha matibabu ya Saratani kwa kutumia mionzi katika Hosipitali ya
Bugando Jijini Mwanza.
Baadhi ya majengo kwa ajili ya
huduma husika yamekamilika yakiwemo jengo ambalo ni maalumu kwa ajili ya
kudhibiti mionzi ambapo ukuta wake umejengwa kwa zege nene la mita
moja,jengo la kutolea huduma za mionzi, baadhi ya wataalamu wapo na
baadhi ya mashine za matibabu kwa mionzi zimeshanunuliwa zikiwemo Cobalt
60 na CT Simulator.
“Takwimu zinaonyesha kuwa katika
kipindi cha mwaka 2009-2017 Hosipitali imetoa matibabu kwa wagonjwa
39,300 kati yao 12,200 wakiwa ni wapya sawa na wastani wa wagonjwa wapya
1500 kwa mwaka” Alisisitiza Dkt. Kigwangala.
Akifafanua Mhe. Kigwangala amesema vifaa vingine ikiwemo brachytherapy na immobilization devices zinatarajiwa kuwasili mwezi Disemba mwaka huu.
Aidha, kwa sasa huduma za Tiba ya
Saratani zinazopatikana katika Hosipitali ya Bugando ni zile za matibabu
yasiyo ya mionzi (chemotherapy) ambazo zilianza januari 2009 kufuatia
Sera ya Serikali kutoa huduma hizo Kikanda.
Kutokana na msongamano wa Wagonjwa
wanaosumbuliwa na Ugonjwa wa Saratani uliopo katika Hospitali ya Ocean
Road pamoja na gharama kwa ndugu wa wagonjwa, Serikali imeadhamiria
kuboresha huduma za Afya kwa kupanua huduma hizo hadi ngazi ya Kanda.
0 comments:
Post a Comment