METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 27, 2017

MWANZA NA MKAKATI WA KUVUTIA UWEKEZAJI

Mkoa wa Mwanza umedhamiria kuvutia Uwekezaji kwa kuondoa vikwazo na changamoto zisizo za lazima kwa kushirikisha taasisi binafsi na za umma ili kuyafikia malengo na sera ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ya kuwa na nchi yenye Uchumi wa Viwanda.

Hayo yamebainishwa na mkuu wa mkoa Mwanza Mhe John Mongela alipokuwa akizindua kitabu kipya kinachoelezea milango ya Uwekezaji mkoani Mwanza hafla iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa ambapo amesema mkoa wake umedhamiria kurahisisha Uwekezaji kwa kuondoa vikwazo na taratibu zote zisizo za lazima zinazokwamisha wawekezaji.

‘… Lakini mie niseme kwenye kitu kimoja ambacho tunatakiwa tubadilike tunafata sana taratibu  ni vizuri kufata taratibu lakini taratibu zipo kwenye kufanikisha mambo yetu, Taratibu zikishakuwa ndio kikwazo ujue hiyo taratibu hata kwenye maisha yako binafsi uachane nayo, Nimewaambia ndugu zangu SUMATRA, EWURA, OSHA, NEMC, TFDA, TBS, BRELA, na FIRE, Sasa nasema kwenye mkoa wa Mwanza tunataka tutengeneza namna nyengine ya kufanya kazi …’ Alisema 

Aidha ameongeza kuwa mkoa wake utaendelea kupambana na suala zima la uharibifu wa mazingira huku akiwakaribisha wafanya biashara walioshiriki hafla hiyo kuja kuwekeza katika mkoa wake  Kwa upande wake muwakilishi wa wabunge wote wa mkoa Mwanza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kumshukuru mkuu huyo wa mkoa pia amempongeza kwa nia yake ya dhati ya kutekeleza kwa vitendo Sera ya Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ya kuwa na nchi yenye uchumi wa viwanda huku akiahidi ushirikiano kutoka kwa wabunge wote wa mkoa wa Mwanza.

Nae mwakilishi wa wafanya biashara wote wa Mkoa Mwanza Ndugu Joseph Kahungwa amemshukuru mkuu huyo wa mkoa huku akiahidi ushirikiano na utekelezaji wa kuutumia vyema mlango alioufungua wa uwekezaji.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wakuu wa wilaya za mkoa Mwanza, wakurugenzi, timu za uwekezaji kutoka wilaya za mkoa Mwanza na wafanyabiashara mbalimbali.

‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’  Imetolewa na Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
28.11.2017

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com