Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi,Vijana na Ajira)
Mh Anthony Mavunde leo amefanya ziara ya ukaguzi wa masuala ya kazi na
kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi mkoani
Kilimanjaro.
Mavunde alianza ziara hiyo katika shule ya Kimataifa ya Moshi
(ISM) ambapo alisikiliza kero za wafanyakazi na kutoa maagizo kwa Menejimenti
ya Uongozi wa Shule hiyo kutoa mikataba kwa wafanyakazi kwa mujibu wa kifungu
cha 14 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini kinavyoelekeza ikiwa ni pamoja
na kuagiza Taasisi za Serikali kuchunguza malalamiko juu ya unyanyasaji kwa
wafanyakazi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa menejimenti.
Naibu Waziri Mavunde amewaagiza Afisa Kazi Mfawidhi na Afisa wa
Uhamiaji wa mkoa wa Kilimanjaro kuzichukua hati za kusafiria za raia wa kichina
9 mpaka watakapowasilisha Vibali vya kufanya kazi nchini na Vibali vya makazi.
Aidha Mavunde alitembelea Kiwanda cha China Paper Corporation
ambapo alisikiliza kero za wafanyakazi na kuiagiza Menejimenti ya Kiwanda hicho
kuhakikisha sheria za Kazi zinafuatwa kwa kutoa Mikataba kwa wafanyakazi wote
na kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa ikiwemo usalama wa mazingira ya
kufanyia kazi.
0 comments:
Post a Comment