METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 12, 2017

KIWANDA CHAWAFUATA WAKULIMA WA NYANYA ILULA











KILIO cha ukosefu wa soko la nyanya linalowakabili wakulima wa mji mdogo wa Ilula na maeneo yanayozunguka wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kimeanza kupata ufumbuzi baada ya kiwanda cha Dabaga Vegetable kutangaza kununua tani 10 hadi 20 za zao hilo kwa siku.
Kiwanda hicho ambacho awali kilikuwa mjini Iringa, kimejengwa upya na kuanza uzalishaji hivikaribuni katika kijiji cha Ikokoto kata ya Ilula wilayani Kilolo, kikiwa kimetanuliwa ukubwa wake.
Mtaalamu wa ubora wa bidhaa za kiwanda cha Dabaga, Zainabu Miraji alisema uwezo wa kiwanda ni kuzalisha tani 40 za nyanya kwa siku, lakini kimeanza kununua kati ya tani 10 na 20 tu kwa siku kwa kuzingatia mahitaji ya masoko yao kwasasa.
“Nyanya tunayohitaji ni ile yenye ubora wa daraja B iwe imekomaa ikiwa shambani, nyekundu iliyoiva, isiwe na madoa meusi, isiwe na fangasi na wala imetobolewa na wadudu,” alisema.
Akizungumza na baadhi ya wakulima wa nyanya wa kata hiyo waliokuwa wakishiriki siku ya wakulima kiwandani hapo jana, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah aliipongeza kampuni mama ya kiwanda hicho ya Chai Bora akisema uamuzi wao wa kujenga kiwanda hicho karibu na wakulima ni utekelezaji wa azma ya Rais Dk John Magufuli ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
“Wilaya ya Kilolo ni moja ya wilaya chache zinazozalisha nyanya kwa kiwango kikubwa nchini. Kiwanda hiki kitasaidia kwa kiwango fulani kupunguza upotevu wa nyanya zilizokuwa zikioza kwasababu ya ukosefu wa soko,” alisema.
Ili kiwanda hicho kizalishe kwa kiwango chake na kifikirie kupanua uzalishaji wake, Abdallah alisema wakulima na wananchi wa wilaya hiyo wanawajibu wa kusaidia kutangaza bidhaa zake ili zipate masoko mengi zaidi.
Aliwataka wakulima wa mazao yanayohitajika kiwandani hapo kuzalisha kwa kuzingatia ushauri na utaalamu unaotakiwa ili wapate bidhaa zitakazopata soko la uhakika.
Mmoja wa wakulima wa nyanya katika kata hiyo, Yohanes Mhanda alikiomba kiwanda hicho kizalishe kwa kiwango chake ili wakulima wauze zaidi na akasema wanao uwezo wa kuboresha kilimo hicho kwa kuzingatia vigezo vilivyotolewa.
Akizungumzia uzalishaji wa nyanya katika wilaya hiyo, Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula, Edward Mbembe alisema wilaya inazalisha tani 55,000 hadi 70,000 za nyanya kwa misimu miwili kila mwaka.
“Msimu wa kwanza ni wa kati ya Novemba hadi Desemba na msimu wa pili ni wa kati ya Machi hadi Juni. Kwa ujumla tuna siku 180 za uzalishaji kila mwaka,” alisema.
Alisema kama uwezo wa kiwanda utakuwa ni kununua tani 10 kwa siku, basi kwa siku 180 kitanunua tani 1,800 na kama ni tani 20 basi kwa siku hizo kitanunua tani 3,600.
 “Kiwanda kitapunguza tatizo la soko, lakini pia tusibweteke, ni lazima tuendelee kutafuta masoko mengine na hayo tuliyonayo tuyaimarishe zaidi,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com