Naibu
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiongozana na Mkuu wa Chuo
cha Maji (WDMI), Dkt. Shija Kazumba wakielekea kwenye moja ya maabara ya
chuo hicho katika ziara yake chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso akipokea maelezo kutoka kwa mtaalamu wa maabara
ya ubora wa maji, Livingston Swila alipofanya ziara Chuo cha Maji
(WDMI).
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Maji (WDMI) katika ziara yake chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji
wa DDCA, Jonathan Mgaiwa (kushoto) alipotembelea taasisi hiyo.
Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso akizungumza na wafanyakazi wa DDCA (hawamo
pichani), akiwa pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu Wizara
ya Maji na Umwagiliaji, Visensia Kagombora (kushoto), Mkurugenzi
Mtendaji wa DDCA, Jonathan Mgaiwa (kulia) na Meneja Biashara DDCA,
Domina Msonge (mwisho kulia).
………………
Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso ameitaka Wizara ya Maji na Umwagiliaji na
wananchi kwa ujumla kuwatumia Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa
Mabwawa (DDCA) ipasavyo ili kuleta maendeleo kwenye Sekta za Maji na
Umwagiliaji nchini kutokana na uwezo mkubwa ilionao.
Hayo ameyasema wakati akiongea na
wafanyakazi wa DDCA wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika taasisi
hiyo kwa lengo la kujionea utendaji na changamoto zao za kikazi, na
jinsi ya kuiongezea uwezo taasisi hiyo katika kufanikisha utimizaji wa
majukumu yake kwa ufanisi.
‘‘Tumekua tukilalamika kuhusu
utendaji mbovu wa makampuni mengi, ambayo yamekuwa yakilipwa fedha
nyingi bila kukamilisha miradi ya visima na mabwawa na kuigombanisha
Serikali na wananchi wake. Wakati tuna DDCA ambao wana uwezo mkubwa na
wamekuwa wakifanya kazi nzuri,’’ alisema Aweso.
‘‘Umefika wakati wa kuwatumia DDCA
kwenye kazi zetu za uchimbaji visima na ujenzi wa mabwawa, hawa kwa
kiasi kikubwa watakuwa mwarobaini wa changamoto za maji kwa maeneo
ambayo wananchi wake wana kilio cha huduma ya majisafi na salama, na
kama wizara tutawajengea uwezo ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi’’
alisisitiza Aweso.
Aidha, Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, alitembelea Chuo cha Maji (WDMI) kwa lengo la kujua
maendeleo ya chuo hicho kikongwe nchini chenye sifa ya kutoa Wataalamu
wa Sekta ya Maji nchini kwa muda mrefu.
Akiwa Chuo cha Maji amejionea
uhalisia wa chuo hicho, ikiwemo changamoto zinazokikabili na kuzungumza
na uongozi wa chuo pamoja na wanafunzi.
Akizungumza chuoni hapo alisema
kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha inakijengea uwezo chuo hicho, kwani
wataalamu wake ndio wanaokwenda kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji
nchi nzima, lakini pia kuhakikisha wanaajiriwa mara baada ya kumaliza
masomo, ikizingatiwa kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wizarani kwa
sasa.
Aweso ambaye amekuwa Naibu Waziri
wa Maji na Umwagiliaji wa kwanza kutembelea taasisi hiyo tangu
ianzishwe, alisema kuwa amezipokea changamoto zote na kuahidi kuzifanyia
kazi, ili wataalamu wanaotoka chuoni hapo wawe faida kwa taifa,
hususani kutatua changamoto ya huduma ya maji inayokabili wakazi wa
maeneo mbalimbali nchini.
0 comments:
Post a Comment