Wednesday, November 22, 2017

DDCA IKITUMIWA VIZURI, ITAKUWA MWAROBAINI WA CHANGAMOTO YA MAJI NCHINI-AWESO

1Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiongozana na Mkuu wa Chuo cha Maji (WDMI), Dkt. Shija Kazumba wakielekea kwenye moja ya maabara ya chuo hicho katika ziara yake chuoni hapo.
2
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akipokea maelezo kutoka kwa mtaalamu wa maabara ya ubora wa maji, Livingston Swila alipofanya ziara Chuo cha Maji (WDMI).
3
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Maji (WDMI) katika ziara yake chuoni hapo.
4
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa DDCA, Jonathan Mgaiwa (kushoto) alipotembelea taasisi hiyo.
5
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akizungumza na wafanyakazi wa DDCA (hawamo pichani), akiwa pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Visensia Kagombora (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa DDCA, Jonathan Mgaiwa (kulia) na Meneja Biashara DDCA, Domina Msonge (mwisho kulia).
………………
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ameitaka Wizara ya Maji na Umwagiliaji na wananchi kwa ujumla kuwatumia Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ipasavyo ili  kuleta maendeleo kwenye Sekta za Maji na Umwagiliaji nchini kutokana na uwezo mkubwa ilionao.

Hayo ameyasema wakati akiongea na wafanyakazi wa DDCA wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika taasisi hiyo kwa lengo la kujionea utendaji na changamoto zao za kikazi, na jinsi ya kuiongezea uwezo taasisi hiyo katika kufanikisha utimizaji wa majukumu yake kwa ufanisi.

‘‘Tumekua tukilalamika kuhusu utendaji mbovu wa makampuni mengi, ambayo yamekuwa yakilipwa fedha nyingi bila kukamilisha miradi ya visima na mabwawa na kuigombanisha Serikali na wananchi wake. Wakati tuna DDCA ambao wana uwezo mkubwa na wamekuwa wakifanya kazi nzuri,’’ alisema Aweso.

‘‘Umefika wakati wa kuwatumia DDCA kwenye kazi zetu za uchimbaji visima na ujenzi wa mabwawa, hawa kwa kiasi kikubwa watakuwa mwarobaini wa changamoto za maji kwa maeneo ambayo wananchi wake wana kilio cha huduma ya majisafi na salama, na kama wizara tutawajengea uwezo ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi’’ alisisitiza Aweso.

Aidha, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, alitembelea Chuo cha Maji (WDMI) kwa lengo la kujua maendeleo ya chuo hicho kikongwe nchini chenye sifa ya kutoa Wataalamu wa Sekta ya Maji nchini kwa muda mrefu.

Akiwa Chuo cha Maji amejionea uhalisia wa chuo hicho, ikiwemo changamoto zinazokikabili na kuzungumza na uongozi wa chuo pamoja na wanafunzi.

Akizungumza chuoni hapo alisema kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha inakijengea uwezo chuo hicho, kwani wataalamu wake ndio wanaokwenda kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji nchi nzima, lakini pia kuhakikisha wanaajiriwa mara baada ya kumaliza masomo, ikizingatiwa kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wizarani kwa sasa.

Aweso ambaye amekuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa kwanza kutembelea taasisi hiyo tangu ianzishwe, alisema kuwa amezipokea changamoto zote na kuahidi kuzifanyia kazi, ili wataalamu wanaotoka chuoni hapo wawe faida kwa taifa, hususani kutatua changamoto ya huduma ya maji inayokabili wakazi wa maeneo mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment